Shikhalo Yanga ni njia tu

Muktasari:

Mwanaspoti limefanya mahojiano na Shikhalo ambaye amezungumzia maisha yake klabuni Yanga tangu atue.

UKITAJA jina la Farouk Shikhalo hivi sasa kwa mashabiki wa Yanga ni mwendo wa kupiga makofi tu na hilo limezidi baada ya kuokoa michomo mingi katika ‘Derby ya Kariakoo’ dhidi ya Simba iliyopigwa Januari 4 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Shikhalo alianza kupigiwa hesabu baada ya aliyekuwa kipa wao Beno Kakolanya kugoma kucheza akidai kulipwa pesa zake za usajili pamoja na mishahara.

Baada ya ‘Derby ya Kariakoo’ mashabiki wa Yanga kila mmoja amefurahishwa na kiwango chake, wakati upande wa Simba wakimtupia lawama kipa wao Aishi Manula kwa magoli anayofungwa.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na Shikhalo ambaye amezungumzia maisha yake klabuni Yanga tangu atue.

ATUA YANGA PRESHA JUU

Shikhalo anasema baada ya kupokea ofa ya kuja Yanga ilibidi aangalie kwa undani klabu hiyo kupitia historia, baadaye akagundua kwamba klabu ya Yanga ni kubwa kuliko klabu yake ya zamani Bandari FC.

“Presha ilikuwepo kwasababu nilikuwa nakuja sehemu mpya kwangu kwahiyo nilikuwa najua nakuja kwenye klabu kubwa kuliko ninayotoka hivyo nilikuwa nahitaji utulivu wa akili zaidi.”

Kipa huyo alisema baada ya kukaa kwa muda mfupi nchini amegundua mashabiki wa Yanga ndio nguzo muhimu katika klabu hiyo kwani wanajitoa kwa hali na mali.

“Mashabiki wa Yanga wao ndio nguzo ya klabu, wao ndio wanafanya sisi tujitume kwasababu tukipata matokeo mabovu wanaumia kwahiyo hali hiyo inatufanya sisi tujitume.”

ISHU YA KAKOLANYA

Kakolanya alijichukulia umaarufu zaidi katika mchezo wa raundi ya kwanza akiwa na Yanga walipocheza na Simba katika msimu uliopita, mashabiki wa Yanga walijikuta wakishindwa kuzuia hisia zao kwake.

Ghafla kipa huyo aliamua kuwakacha akisisitiza kulipwa pesa zake, na hapo ndipo Yanga wakaanza kumpigia hesabu Shikhalo na baada ya Afcon 2019 walimpata.

Shikhalo anasema hadi anatua Yanga alikuta sifa za Kakolanya kwamba ni kipa mzuri ambaye ameacha alama yake lakini anaamini na yeye ataacha kitu cha tofauti katika klabu hiyo.

“Kakolanya ni kipa mzuri kwasababu nimekuta kila mtu akimzungumzia, ukiona mtu anakubalika ina maana kwamba alifanya vizuri kwasababu mpaka Yanga ukubalike sio kitu kidogo,” alisema.

METACHA, KABWILI

Pamoja na Shikhalo, Yanga kuna makipa watatu, akiwamo Metacha Mnata na Ramadhan Kabwili, ambao wameonyesha kiwango kizuri, hali inayofanya kocha wa makipa Peter Manyika kuwapanga kwa kumpa nafasi kila mmoja.

Metacha awali alikuwa anacheza mechi za kimataifa wakati Yanga wakishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe Shirikisho Afrika, huku Shikhalo akicheza mechi za Ligi Kuu. Hata hivyo, baada ya Yanga kutolewa katika mashindano hayo wamejikuta wakigawana mechi.

Shikhalo anakiri ushindani wa namba upo lakini anauchukulia kama sehemu yake ya kuendelea kuwa bora zaidi.

“Ushindani huu unanijenga kwasababu makipa wote tupo vizuri hivyo kila anayepewa nafasi anahakikisha anafanya vizuri ili kuendele kupata nafasi katika kikosi cha kwanza,” anasema.

Shikhalo anasema kitu kingine ambacho kinamfanya awe na amani ni upendo uliopo baina ya makipa wote Yanga hali inayowafanya kuwa na amani anapocheza yeyote.

“Tunajituma wote kwa pamoja kwasababu wote tupo katika timu za Taifa, kwahiyo ili kila mmoja aendelee kuwepo katika timu ya Taifa lazima afanye vizuri,” alisema.

TOFAUTI YA YANGA, BANDARI

Shikhalo anasema tofauti kubwa aliyokutana nayo Yanga ni mashabiki kupenda kweli timu yao kiasi cha kujitoa hali na mali kuhakikisha timu yao inafanya vizuri.

“Hapa Yanga wana mashabiki wengi kuliko Bandari na wanapenda mpira kweli kweli, simaanishi kwamba Bandari hawapendi mpira, hapana, lakini hapa wamezidi.”

Kuhusu hali ya hewa anasema: “Unajua mi natokea Mombasa kwahiyo hali ya joto ni sawa tu na kule, hainisumbui.”

DERBY YAMPA MZUKA

Licha ya ugeni wa ‘Derby ya Kariakoo’, Shikhalo alifunika na kujijengea ufalme wake kwa mashabiki wa Yanga na anafunguka: “Mechi hizi zinakuwa ni za kutengeneza au kuharibu, lakini pia ni mchezo wa kubadilisha maisha ya mtu ikitokea amefanya vizuri, katika mchezo ule tulikuwa tunataka matokeo ili kusogea mbele.”

Alisema hata magoli walivyofungwa hayakumkatisha tamaa bali alizidi kujitoa na kuwahamasisha wachezaji wenzake kujitoa zaidi.

WALIPOKOSEA SIMBA

Kuhusu mechi ya Watani wa Jadi iliyomalizika kwa sare 2-2, Shikhalo anasema walichokosea Simba ilikuwa ni kuingia uwanjani wakiwa na matokeo yao.

“Mashabiki wa Simba walikuwa wamejaa uwanjani wakiamini kwamba wanashinda, lakini na sisi tulitaka matokeo ili mashabiki wetu wajitokeze kwenye mechi zetu,” alisema.

“Simba wana wachezaji wazuri, Kagere nimecheza naye takribani mechi 10 tukiwa Kenya, ni mchezaji mzuri na ninamfahamu vizuri kwamba analijua goli,” alisema.

Aliongeza kwa kusema katika mechi hizo kila mchezaji anaweza akafunga na si mchezaji mmoja pekee ambaye anaweza kufanya hivyo tu.

ANAUTAKA UBINGWA

Licha ya Yanga mwanzo mgumu wa msimu, Shikhalo anaamini timu yao inaweza kutwaa ubingwa.

“Bado tuna nafasi ya kuchukua ubingwa msimu huu, timu yetu ipo katika nafasi nzuri lakini inatakiwa kupambana kwasababu ushindani upo wa hali ya juu,” alisema.

Shikhalo aliongeza: “Ukiangalia tulipokuwa tunaanza na hivi sasa tulipo kuna tofauti kubwa mno kwahiyo naamini kila kitu kitaenda kuwa sawa katika msimu huu.”

YANGA HAJAFIKA

Wachezaji wengi wageni wanapokuja nchini kupiga soka wanakuwa na mipango yao mingine ya muda mfupi ili kuweza kuendelea na maisha mengine.

Kwa upande wa Shikhalo naye anasema Yanga hajafika kwasababu bado ana mipango yake mingine ya kucheza soka la kulipwa katika Ligi zenye ushindani zaidi.

“Mchezaji yeyote anayecheza mpira ana ndoto kwahiyo Yanga kwangu sio mwisho, popote ambapo nitapata klabu ya maslahi zaidi nitaondoka naamini Yanga wataniachia,” anasema.

Anasema hawezi kusema ni sehemu gani kwasasa kutokana na safari yake bado ndefu hivyo anachoangalia kwa wakati huu ni timu yake kufanya vizuri kwanza.

UKATA HAUKUMPA PRESHA JANGWANI

Wakati Yanga imekumbwa na ukata huku wachezaji wa kigeni kama Issa Bigirimana, Juma Balinya, Sadney Urikhob na wengineo wakijiweka pembeni kuichezea timu hiyo, lakini hali ilikuwa tofauti kwa Shikhalo.

Kipa huyo anasema hali hiyo haikumtingisha kwa vile aliamini ni hali ya mpito na kwamba kila kitu kitakaa sawa.

“Katika familia kuna wakati mgumu lakini pia kuna wakati mzuri, hali hizi zote inabidi zikukute ukiwa ndani ya familia na ndio maana mimi niliamua kubaki,” alisema.

Kwa upande wa wachezaji wenzake ambao waliamua kuishia njiani, Shikhalo alikiri kwamba ni marafiki zake lakini yeye binafsi hakushirikishwa katika uamuzi wao.

“Mimi nilikuja peke yangu hapa na ndio nikakutana nao hapa, huwa tunazungumza baadhi ya vitu na kupeana ushauri lakini katika hili sikupata bahati ya kushirikishwa.”