Shikamkono afunguka kuhusu Mo Dewji ,achoshwa na visa vya Gaga na Kizota

Muktasari:

Mazungumzo haya yayolifanyika katika Kijiji cha Gomero, Kisaki mkoani Morogoro leo wiki iliyopita yanafikia tamati.

TAKRIBANI wiki nzima tulikuwa tunaangazia mazungumzo kati ya mfadhili, mratibu wa zamani wa Simba, Jabir Ally Shikamkono na mwandishi wetu MOHAMMED KUYUNGA.

Mwishoni mwa miaka ya 80’, Shikamkono alirudi nchini akitokea Urabuni na kiasicha zaidi ya Dola 100,000 anasema pesa nyingi kati ya hizo alizimalizia katika klabu yake pendwa ya Simba ya jijini Dar es Salaam.

Tajiiri huyo wa enzi hizo, alifanya kila kitu kwa ajili ya Simba, kuanzia usajili, kulipa mishahara, posho na kuisafirisha timu katika mikoa mbalimbali wakati huo ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu).

Mazungumzo haya yayolifanyika katika Kijiji cha Gomero, Kisaki mkoani Morogoro leo wiki iliyopita yanafikia tamati.

AMPA SOMO MO DEWJI

Kwanza Shikamkono amefurahi sana kitendo cha Mfanyabiashara, Mohammed Dewji ‘MO’ kuichukua timu hiyo.

“Simba ilimhitaji MO siku nyingi sana, naona kama tulichelewa kumpata,” anasema na kuongeza anaamini baada ya miaka michache ijayo timu hiyo itakuwa inacheza anga za kimataifa tu.

“Kwanza MO ana bahati sana na Simba, kumbuka mwaka 2003 akiwa mdhamini wa klabu hiyo ilifuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mwaka huu pia imefuzu hatua hiyo akiwa mwekezaji.

“Hii ni bahati kubwa saba sio kila mtu anaweza kuwa nayo, nyota yake inang’ara ndani ya Simba ndio maana inapata mafanikio kama hayo,” anasisitiza.

Mbali na kumfagilia MO, Shikamkono anatoa machungu yake kwa kumtaka bosi huyo kuwa mkali kwa mienendo mibovu ya timu hiyo.

“Lazima awe mkali la sivyo itakuwa ni kazi bure na timu itayumba. MO anatakiwa azungukwe na watu wa mpira ambao wana uchungu na klabu sio ambao watakuwa wakituletea wachezaji wa hovyo.”

WACHEZAJI ANAOWATAKA

Shikamkono aliumua sana Simba ilipofungwa mabao 5-0 dhidi ya AS Vita ya DR Congo na hata ilipobugizwa idadi kama hiyo dhidi ya Al Ahly ya Misri kule Alexandra.

“Vipigo vile sikuvitegemea, viliniumiza sana,” anasema Shikamkono na uso wake kutawaliwa na huzuni.

“Sidhani kama wachezaji wanaelewa jinsi mashabiki na wanachama wa Simba wanavyoumia kwa vipigo vile. Hatujazoea kufungwa mabao mengi kama yale tena mara mbili! Ile ilikuwa ni tabia ya watani zetu wa jadi (Yanga),” anasema.

Aidha katika hilo, Shikamkono anamtaka MO kusajili wachezaji wa kimataifa kweli ambao wanaweza kuibeba timu ndani na nje ya nchi.

“Tunahitaji wachezaji wanaozichezea timu zao za taifa ambao wanaweza kutoa upinzani barani Afrika na MO anatakiwa azingatie hilo.”

AWABAKISHA SABA TU

Kama haitoshi, Shikamkono amewapiga mkasi wachezaji kibao waliosajiliwa kukitumikia kikosi hicho na kuwabaakisha saba tu ambao amedai ndio wanaostahili kuichezea timu hiyo.

Bosi wa zamani kwa sasa anaishi maisha ya kawaida kijijini akijihusisha na kilimo, anasema wachezaji wa kigeni wanaostahili kubaki Simba ni Clatous Chama, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere tu.

Kwa upande wa wazawa amewabakisha Aishi Manula (akitaka aongezewe kipa bora wa kumpa changamoto), Jonas Mkude na Erasto Nyoni.

“Tunahitaji wachezaji wa kimataifa wanaotambulika kwao. Hapo MO atakuwa amefanya uwekezaji wa maana kwenye kikosi.”

AMGUSA AUSSEMS

Katika hatua nyingine, Shikamkono amemgusa Kocha wa Simba, Patrick Aussems na kusema kama ataendelea kufanya vibaya atafutwe kocha mwingine bora zaidi yake.

“Tulipofungwa tano za kwanza (kule Congo) nikajua atajifunza kitu katika mechi za ugenini. Inashangaza tunakwenda Misri hatuna game plan tukapigwa tena tano.

“Huyu ni wa kumtathimini kama kweli kiwango chake kinafaa kuendelea kubaki Simba, ngoja tuone mechi zinazokuja,” anasema Shikamkono ambaye mashabiki wa kijijini kwake walijazana nyumbani kwake Simba ilipofungwa na Al Ahly 5-0.

GAGA NA KIZOTA SASA

Shikamkono anawakubali sana wachezaji wa zamani ambao wote ni marehemu kina Hamisi Thobias ‘Gagarino’ na Said Mwamba ‘Kizota’.

“Hawa walikuwa wachezaji wa kweli lakini walikuwa wavivu sana wa mazoezi. Gaga yeye alikuwa anasema yeye ni ‘natural’ hana haja ya kufanya mazoezi ila akiamua kucheza utampenda. Mara kadhaa nilikuwa naitwa kutatua matatizo yake na kina Yussuf Hazali.

“Kizota naye hakupenda kabisa kufanya mazoezi kuna kocha mmoja alitaka kumweka benchi kwenye mechi muhimu, nilimzuia na alipocheza matunda yake aliyaona.

UNAMKUMBUKA DAVID MIHAMBO?

Shikamkono anafichua siri ya mchezaji mwengine wa zamani wa Simba na Reli ya Morogoro David Mihambo.

“Huyu jamaa angekuwa mbali sana kama asingeendekeza starehe. Tulipomsajili Simba alikuwa anapita tu, alitakiwa acheze kwa kiwango ili aende Uholanzi ambako dada yake alishamtafutia timu lakini ndio hivyo,” anasikitika.

Shikamkono anasema alishiriki kumsajili Mihambo ambaye alikuwa straika hatari enzi zake sambamba na kina Adam Selemani na Juma Limonga wote kutoka Reli Morogoro na Dan Mhoja kutoka Pamba ya Mwanza.

“Mihambo alikuwa mzuri sana kwa mashuti ya mbali, alitakiwa kwenda Uholanzi kwa dada kucheza soka kama angefanya vizuri. Dada yake alisikitika sana baada ya Mihambo kushindwa kufanya vizuri.”

KIKOSI CHA CHA SIMBA

Katika kumalizia makala haya, Shikamkono amekitaja kikosi chake bora cha muda wote ndani ya Klabu ya Simba.

Kipa wake ni Mohammed Mwameja, mabeki beki wa kulia ni Kasongo Athumani, beki wa kushoto ni Deo Mkuki (Twaha Hamidu).

Mabeki wa kati ni Mustafa Hoza (Amri Said) na kitasa wake ni George Magere Masatu. Katikati anamuweka Suleimani Matola (Ramadhani Lenny).

“Unajua Matola alikuwa kapteni mwenye mafanikio pale Simba na enzi zake hatukuwahi kufungwa na Yanga hata mara moja,”anakumbusha Shikamkono.

Winga wa kulia George Lucas ‘Gaza) kiungo wa juu ni Hussein Aman Marsha (Clatous Chama). Mshambuliaji ni Madaraka Suleimani ‘Mzee wa Kiminyio’.

“Hili jina la Mzee wa Kiminyio ni mimi ndiye niliyempachika enzi hizo kutokana na uwezo wake wa kufinya na kukaa na mpira,” anasema Shikamkono na kuachia tabasamu.

Nteze John ‘Lungu’ na Dua Said na wanatokea benchi ni Ulimboka Mwakingwe na Thomas Kipesye.