Shangwe za mashabiki TFF zawashtua polisi

Muktasari:

Kesi ya Morrison bado haijatolewa majibu mpaka sasa hali inayofanya mashabiki wapatwe na shauku kubwa.

KUCHELEWA kutoka kwa maamuzi ya kikao cha Kamati ya Sheria, Hadhi na Haki za wachezaji juu ya hatma ya mchezaji Benard Morrison kumewafanya mashabiki waanze kupiga kelele za kutaka majibu ya kesi yatoke.

Mashabiki hao walipoanza kuimba nyimbo za kuonyesha kuchoka kusubiri majibu, kuliwafanya askari polisi wawatawanye na kutengeneza njia ya magari kupita kwa usalama.

Awali licha ya mashabiki kuimba, Polisi waliokuwepo eneo hilo wakiimarisha ulinzi hawakuonyesha ukali kwa mashabiki hao bali waliwataka kutokatibia geti la kuingilia ofisi za TFF.

Polisi waliwasha magari yao mawili waliyokuwa wameyaegesha pembeni mwa geti na kutoka kuweka karibu na kona ya kuingilia geti la ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zilizopo Karume jijini Dar es Salaam.

Baada ya Polisi kufanya hivyo mashabiki hao waliendelea kupiga shangwe mbalimbali.

"Senzo, Senzo, Senzo, Yanga, Yanga, Yanga," walisikika mashabiki hao waliokuwa wamejitokeza huku wakionekana kutokuwa na presha yoyote pamoja na kutulizwa na polisi hao.

GARI LA TATU LAONGEZWA

Baada ya shangwe kuzidi gari lingine la Polisi (la tatu) liliongezwa likuwa na askari wawili waliokuwa wameshika risasi za moto.

Gari hilo baada ya kuingia lilienda moja kwa moja ndani kisha likageuza na kwenda kukaa mbele ya gari zingine mbili za polisi huku askari wawili wakiwa wapo juu.