Shamte: Tunatesti mitambo Azam FC

Muktasari:

Beki wa Simba anaamini Azam FC itakuwa kipimo chao kujiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo ambao walitoka nao suluhu kwao.

BEKI wa Simba, Haruna Shamte amesema mechi ya ngao ya jamii na Azam FC ndio itakayowapa taswira ya nini watakivuna kwenye marudiano na UD Songo baada ya kusuluhu ugenini.
Shamte amesema uwezo walionao wachezaji wa Azam FC anaamini utawajenga kiuwezo na kimbinu kujua namna ya kushinda mechi ya marudiano na UD Songo.
"Azam FC ni timu yenye ushindani wa hali ya juu, kwetu kitakuwa ni kipimo cha kutuandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa na UD Songo ingawa na wao itakuwa ya kuwaandaa na Ethiopia, hivyo ushindani utakaokuwepo kwetu utakuwa kipimo.
"Baada ya matokeo ya suluhu ugenini mashabiki wa Simba wanatamani kuona tunafanya kitu kwenye uwanja wa nyumbani ambako watakuja kutuunga mkono, hatuna budi kupambana kwa namna yoyote ile kupata matokeo," amesema.
Amesema kujipima na timu ambayo ni washindani wao kwenye ligi kuu Bara, anaamini kunatosha kuwaonyesha mwanga wa nini wafanye kwenye mchezo mgumu wa kimataifa uliopo mbele yao.