Shahidi akwamisha kesi ya Wema yapigwa kalenda

Muktasari:

  • Wema anadaiwa Oktoba 15 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam alirekodi video ya ngono na kuisambaza katika mtandao wake wa Instagram.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka katika kesi ya kurekodi video ya ngono na kuisambaza katika mitandao ya kijamii inayomkabili Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu kuleta mashahidi wengi kadri inavyowezekana.

Hayo yalielezwa leo na Hakimu Mkazi, Maira Kasonde baada ya wakili wa serikali Glori Mwenda kudai mahakamani hapo kuwa shahidi aliyekuwa ameandaliwa yuko safarini Arusha kikazi.

“Kesi hii imekuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa na leo tulitakiwa kuwa na shahidi, lakini yuko safarini Arusha kikazi hivyo tunaomba tarehe nyingine kwaajili kuendelea,”alidai Wakili Mwenda

Wakili wa utetezi Ruben Semwanza alidai kuwa hawana pingamizi kama shahidi hayupo, lakini wawe na mawasiliano na shahidi kama hayupo waje mashahidi wengine.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Kasonde aliutaka upande wa mashtaka kuleta mashahidi wengi kadri wanavyowezakana na kuahirisha kesi hiyo Aprili 18 mwaka huu itakapoendelea.

Katika kesi hiyo, Wema anadaiwa Oktoba 15 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam alirekodi video ya ngono na kuisambaza katika mtandao wake wa Instagram.