Shahidi aeleza fedha za Simba zilivyohamishwa

Muktasari:

Mbali na Watera, shahidi mwingine aliyekwisha toa ushahidi katika kesi hiyo kama shahidi wa kwanza ni Boaz Lubila (45) kutoka Benki ya CRDB makao makuu.

MENEJA wa Biashara katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe, George Watera (42) ameileza Mahakama ya Hakimu MKazi Kisutu jinsi aliyekuwa Rais wa Simba, Evans Aveva, makamu wake, Godfrey Nyange na Amos ambaye ni Mhasibu walivyofika ofisini kwake na kuhamisha Dola 300, 000 kutoka akaunti ya Simba Sports iliyopo kwenye tawi hilo kwenda akaunti namba 047002211 iliyopo benki ya Barclays.

Shahidi huyo wa pili wa upande wa mashtaka alieleza hayo jana wakati akiongozwa na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Leonard Swai, kutoa ushahidi wake dhidi ya kesi inayowakabili, Aveva na Nyange inayosikilizwa kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Hata hivyo, shahidi huyo alidai anayeonekana kwenye nyaraka za benki ikiwemo hundi za malipo na mmiliki wa akaunti namba 047002211 ya benki Barclays ni Francis Aveva na sio Evans Aveva.

Watera alidai kuwa Machi 15, 2016 akiwa ofisini kwake akiendelea na majukumu walifika wateja watatu kutoka Simba Spots Club ambao ni Aveva, Nyange na Amos waliikwenda kwa nia ya kuhamisha fedha Dola 300,000 kutoka akaunti ya Simba iliyopo benki ya CRDB kwenda katika akaunti ya Francis Aveva iliyopo benki ya Barclays.

Alidai kuwa wateja hao walipofika benki ya CRDB tawi la Azikiwe walijaza fomu na kuandika maelezo ya Simba Spots Club.

Pia, waliandika sababu za fedha hizo kuhamishwa kwa akaunti hiyo iliyokuwa na jina la Fransis Aveva ilikuwa ni kwa ajili ya malipo ya mkopo ambapo, Simba Sports Club ilikuwa ikimlipa Francis Aveva kupitia akaunti yake namba 047002211.

Alibainisha kuwa katika tukio hilo watia saini wa Simba walikuwa ni Evans Aveva, Godfrey Nyange na Amos.

Baada ya kutoa ushahidi huo Watera aliulizwa na wakili wa upande wa utetezi Nestory Wandiba kuwa, ni jina gani linaoneka katika nyaraka za fomu za kufungulia mkopo benki pamoja na hundi ya malipo ya Dola 300,000.

Akijibu swali hilo Watera alidai kuwa jina linoonekana katika nyaraka hizo ni la Fransis Aveva na kwamba, yeye hamuelewi huyo mtu.

Hata hivyo, Hakimu Simba naye alimuuliza shahidi huyo iwapo anamjua Fransis Aveva, lakini alieleza kuwa hamjui.Kesi hiyo imeahirishwa hadi leo ambapo mashahidi wa upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

Mbali na Watera, shahidi mwingine aliyekwisha toa ushahidi katika kesi hiyo kama shahidi wa kwanza ni Boaz Lubila (45) kutoka Benki ya CRDB makao makuu.

Aveva na Nyange wanakabiliwa na mashtaka mengine zaidi ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha hizo bila mamlaka ya Kamati ya Utendaji ya Simba, kujipatia pesa isivyo halali (Aveva) na utakayishaji fedha yanayowakabili wote, Aveva na Kaburu.

Katika kesi hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe anakabiliwa na mashtaka mawili, ya kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uwongo yeye pamoja na wenzake.