Shahidi aeleza Takukuru walivyozuia mizigo ya Simba

Muktasari:

Mbali na Hans Poppe washtakiwa wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu huyo Evance Aveva, na aliyekuwa Makamu wa wake, Geofrey Nyange maarufu (Kaburu)

Dar es Salaam. Shahidi wa tano katika kesi inayowakabili vigogo wa klabu ya Simba ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) walivyobaini udanganyifu katika mizigo ya klabu hiyo.

Ushahidi huyo Meneja operesheni wa kampuni ya Wafen Tanzania Limited, Jovin Kalinga aliyasema hayo akiongozwa na Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba Kalinga alidai alishawahi kufanya kazi na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu Simba, Zacharia Hans Pope.

Alidai kuwa Hans Pope alikuwa na ofisi yake binafsi anayoagiza mizigo na kampuni yao ilikuwa ikiitoa.

Alidai kuwa Hans Pope alimweleza kuna kazi iko klabu ya Simba ambapo kuna kontena tatu za kutoa bandarini hivyo awasailiane na klabu ya Simba ili kupatana.

"Niliwasiliana na bosi wangu kumweleza na yeye akawasiliana na klabu ya Simba alikwenda kuchukua nyaraka hizo na kuzileta ofisini na kunipa maelekezo ya kufanya," alidai Kalinga

Alidai kuwa katika ufanyaji kazi nyaraka hizo huwa zinatumwa kwenda Mamlaka ya Mapatoa Tanzania (TRA) kwa mtandao na wao kurudisha majibu kwa mfumo huohuo baada ya kuzifanyia kazi nyaraka zilizotoka kwa mteja.

"Baada ya kupeleka TRA hati ya malipo ilikuwa Dola 41000 na majibu yaliokuja walitakiwa kulipa 82 milioni ambapo tuliipeleka Simba kwaajili ya malipo" alidai shahidi huyo

Shahidi huyo alidai baada ya malipo kazi ililikuwa kwenda kuitoa mizigo hiyo, lakini walipofika msimamizi aliwaeleza mizigo imezuiliwa.

Aliendelea kudai wakati wanaondoka alipigiwa simu na mtu aliejitambulisha kwa jina moja la Salim nakumweleza kuwa waache anakwenda kufuatilia Takukuru kisha akamfahamisha Mkurugenzi.

"Tulienda Takukuru na kumkuta mtu aliejitambulisha kwa jina la Frank akauliza mnafahamu nini kuhusu mzigo wa Simba nikamjibu mhusika ndio mteja wetu.

"Walihitaji nyaraka kisha tukaenda kuleta faili tulianza kutoa nyaraka moja baada ya nyingine kisha kuzifananisha baada ya kumaliza waliuliza kama tunafahamu hatia ya malipo ya Dola 100000" alieleza

Shahidi huyo alieleza anafahamu hati ya malipo ya Dola 42000 na tulipoangalia namba za hati hizo zikawa zinafanana tukarudi ofisini kusubiri majibu ya Takukuru.

Akihojiwa na Wakili wa utetezi, Wabeya Kung'e, alidai mzigo ulikuwa wa Simba, hakuna nyaraka yoyote inayoonyesha kwamba Aveva na Kaburu walikabidhi nyaraka yoyote kutoka Simba kwenda Wafem.

Anadai nyaraka za kutoa mzigo wa Simba alizipokea Juni 6 mwaka 2016, maelezo Takukuru aliyatoa kuhusiana na nyaraka yenye thamani ya Dola za Marekani 40,577, lakini anashangaa hakuyaona maelezo yake kutolewa Mahakamani.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 19, mwaka huu kwaajili ya kuendelea na usikilizwaji.

Mbali na Hans Poppe washtakiwa wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu huyo Evance Aveva, na aliyekuwa Makamu wa wake, Geofrey Nyange maarufu (Kaburu).

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 10 ikiwemo kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, kutoa maelezo ya uongo na utakatishaji wa fedha.

Katika shtaka la utakatishaji fedha linalomkabili Aveva, inadaiwa Machi 15, 2016 katika benki ya Barclays Mikocheni, Dar es Salaam alijipatia Dola za Kimarekani 187,817, takriban Sh. Milioni 400 kutoka katika Timu ya Simba wakati akijua zimetokana na zao la kosa la kughushi.

Katika shtaka la kughushi linawakabili washtakiwa wote, ambapo wanadaiwa katika tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zinathamani ya dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh. Milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli.

Pia katika shtaka lingine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya March10 na September 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.