Shahidi: Aveva alikiuka uamuzi wa Kamati Tendaji ya Simba

Thursday July 11 2019

By Hadija Jumanne

Dar es Salaam. Mchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Frank Mkilanya(45) ameieleza Mahakama, jinsi aliyekuwa rais wa Simba, Evans Aveva na wenzake, walivyokiuka maagizo ya yaliyotolewa na Kamati Tendaji ya Klabu hiyo ya kufungua akaunti maalumu kwa ajili ya kutunza fedha, kiasi cha dola za kimarekani 319,212 zilizotokana na uhamisho wa mchezaji wao, Emmanuel Okwi.

Mkilanya ameieleza hayo leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkazi Kuu, Thomas Simba, wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya viongozi wa klabu ya Simba, wanaokabiliwa na kesi ya kughushi na kutakatisha fedha.

Viongozi hao ni aliyekuwa rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva, Makamu wa wake, Geofrey Nyange maarufu Kaburu na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.

Mkilanya ni shahidi wa saba katika kesi hiyo, alidai kuwa washtakiwa hao walikiuka maagizo yaliyotolewa na Kamati hiyo ya kutaka fedha hiyo iliyolipwa Klabu ya Simba kutoka Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya nchini Tunisia, ifunguliwe akaunti maalum, lakini wao waliihamisha fedha hiyo kwenda katika akaunti ya mtu  binafsi.

Akiongozwa na wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai, Shahidi huyo alidai kuwa, Machi 14, 2016 Kamati ya Utendaji wa Klabu, iliitisha kikao kuhusiana na ufunguaji wa akaunti maalum kwa ajili ya kuweka fedha kiasi cha Dola za kimarekani 319,212, ambazo zilipwa na Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya nchini Tunisia ikiwa ni ada ya uhamisho wa mchezaji Emmanuel Okwi kwenda katika  Klabu hiyo.

Shahidi huyo alidai kuwa kikao hicho cha Kamati ya Utendaji, kilipendekeza fedha hizo ambazo ni ada ya uhamisho wa Okwi, zitumike katika ujenzi wa uwanja wa Mpira wa klabu hiyo, uliopo Bunju Manispaa ya Kinondoni pamoja na kumlipa HansPope ambaye alikuwa anaidai klabu hiyo, dola za kimarekani 17,000.

Advertisement

"Siku mmoja baada ya kikao hicho cha Kamati Tendaji ya Klabu ya Simba kuitishwa, Machi  15, 2016, Fedha hizo zilihamishwa kutoka akaunti ya Klabu ya Simba kwenda akaunti binafsi, inayomilikiwa na Aveva" alidia Shahidi huyo na kuongeza.

"Uchunguzi wetu ulibaini kuwa fedha hizo zilizoingizwa katika akaunti ya Aveva, zilitolewa na kutumika sehemu isiyojulikana" alidai Mkilanya, ambaye ana shahada ya kwanza ya uchumi aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam.

Alidia kwa mujibu wa uchunguzi waliofanya, walibaini kuwa dola za kimarekani 62,000 kutoka katika akaunti ya Aveva, zilitumwa nchini China kwa ajili ya uagizaji wa nyasi bandia, huku dola za kimarekani 50,000 zikitumika kumlipa mkandarasi anayejanga uwanja wa Mpira wa Klabu hiyo.

Mkilanya ambaye ameajiriwa Takukuru tangu mwaka 2002, alidai kuwa alipewa kazi na bosi wake ambaye ni Mkurugenzi wa Uchanguzi, afanye uchunguzi kuhusiana na fedha zilizohamishwa kutoka akaunti ya Klabu ya Simba ambazo ni dola za kimarekani 300,000 kwenda katika akaunti ya mtu binafsi, ambayo inamilikiwa na Aveva.

"Nilianza uchunguzi wa kuomba nyaraka za benki ( bank statement) kutoka benki ya CRDB inayomilikiwa na Klabu ya Simba na nyaraka za benki kutoka benki ya Barclays inayomilikiwa na Aveva" Alidia Shahidi.

Alidai pia aliomba fomu za kuhamisha fedha ili kuona nani alihamisha fedha hizo na kwa malengo gani.

"Pia niliomba nyaraka kutoka Klabu ya Simba ambazo zitatuonyesha fedha hizo zilitoka wapi? zilikuwa ni kwa ajili ya shughuli gani na zilipaswa kitumikaje? Na sasa  zilitumikaje" alidia Shahidi hiyo.

Alifafanua kuwa baada ya kufanya uchuguzi walibaini kuwa Avena na Nyange ndio walihusika kuhamisha fedha hizo kutokana na sahihi zao katika nyaraka hizo.

" Nyaraka kutoka benki ya CRDB zilitusaidia kujua watiaji sahihi ambao ni Aveva na Nyange kwa sababu kila nyaraka ilikuwa na majina yao, sahihi zao na picha zao" alidia Shahidi.

Wakati huo huo, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Nehemia Nkoko umepinga maelezo ya onyo aliyotoa Aveva Polisi yasipokelewe na mahakamani hapo kama ushahidi kutokana na kwamba yalichukuliwa kinyume cha sheria.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 16, mwaka hui atakapotoa uamuzi kuhusiana na vielelezo hicho.

Tayari mashahidi saba wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 10, yakiwemo ya kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uwongo na matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha hizo bila Kamati ya Utendaji ya Simba,kukaa kikao.

Katika mashitaka la kughushi linawakabili washitakiwa wote, anadaiwa katika tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zinathamani ya dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli.

Pia katika mashitaka mengine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya Machi 10 na Septemba 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.

Advertisement