Shabiki mbishi atinga Misri

Muktasari:

Lakini Zhakata aliamua kukomaa na kufanikiwa kupenya Ethiopia na kuingia Sudan ambako nako alikutana na changamoto za kuchelewa kupata Viza ya kuingia Misri lakini baada ya subira ya siku 20 kwenye nchi hizo, ndoto yake ilitimia kwa kuingia nchini humo Jumatano iliyopita.

BAADA ya safari ya misukosuko iliyodumu kwa siku 50, shabiki wa soka raia wa Zimbabwe, Alvin Zhakata ametimiza ndoto yake ya kushuhudia Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) baada ya kuwasili Misri juzi, Jumatano.
Zhakata na mwenzake Botha Msila walipanga kusafiri kwa kutumia usafiri wa barabara kutoka Cape Town, Afrika Kusini hadi Cairo, Misri ikiwa ni kampeni maalum ya kuhamasisha mashabiki wa soka Afrika kufuatilia fainali hizo.
Hata hivyo baada ya kuvuka nchi za Zimbabwe, Zambia, Tanzania na Kenya, wawili hao walikutana na kizuizi nchini Ethiopia, jambo lililomlazimisha Botha Msila kughairi na kuamua kupanda ndege kwenda Misri.
Lakini Zhakata aliamua kukomaa na kufanikiwa kupenya Ethiopia na kuingia Sudan ambako nako alikutana na changamoto za kuchelewa kupata Viza ya kuingia Misri lakini baada ya subira ya siku 20 kwenye nchi hizo, ndoto yake ilitimia kwa kuingia nchini humo Jumatano iliyopita.
"Nina zaidi ya fahari kwea kufanya jambo ambalo mwingine asingeweza kuthubutu kufanya. Nitafanya hivyo tena kama nitapata nafasi.
Nasikitika kwamba nimefika hapa baada ya Zimbabwe kutolewa lakini ningejisikia vibaya zaidi kama ningekuwa nimekata tamaa," alisema Zhakata.