Sevilla yamfungia kazi Alvaro Morata

Wednesday January 9 2019

 

Madrid, Hispania. Sevilla imeongeza kasi ya kutaka saini ya mshambuliaji wa Chelsea, Alvaro Morata.

Klabu hiyo ya Ligi Kuu Hispania, imetuma maombi ya kutaka kumsajili Morata katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwakani.

Wakala wa mchezaji huyo Juanma Lopez juzi alikuwa Hispania kuzungumza na klabu hiyo kuhusu uhamisho wa nyota huyo wa zamani wa Juventus ‘Kibibi Kizee’ cha Turin.

Hata hivyo, hakuna taarifa iliyotolewa kuhusu mazungumzo kati ya Lopez na Mkurugenzi wa Ufundi wa Sevilla Joaquin Caparros.

Kocha wa Sevilla Pablo Machin anataka huduma ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania ili kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.

Sevilla ina matumaini ya kunasa saini ya nyota huyo baada ya kushindwa kupata namba katika kikosi cha kwanza chini ya Kocha Maurizio Sarri.

Licha ya kukosa nafasi ya kucheza, lakini Morata amekuwa shujaa wa Chelsea katika mechi anazocheza. Jumamosi iliyopita alifunga mabao mawili katika mchezo wa Kombe la FA.

Morata amefunga mabao tisa katika mechi 24 alizocheza msimu huu. Nguli wa zamani wa Chelsea aliyefunga mabao 70 Gianfranco Zola amemtaka nyota huyo kukabiliana na presha katika kikosi hicho.

“Unacheza Chelsea siyo Southampton au Brighton, unapaswa kukabiliana na ushindani na presha kutoka kila kona,”alisema Zola, mshambuliaji nyota wa zamani wa Italia.

Advertisement