Sevilla FC, Simba SC hapatoshi

Muktasari:

Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas alisema mechi hiyo ni sehemu ya uwajibikaji wa kampuni yao katika kuendeleza soka nchini.

Dar es Salaam. Klabu ya Simba leo inaingia katika historia nyingine katika medani ya soka nchini kwa kucheza na timu ya Hispania, Sevilla FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo imeandaliwa Kampuni ya SportPesa Tanzania, imepangwa kuanza saa 1:00 usiku na Simba inakuwa timu ya kwanza Tanzania kucheza na magwiji hao wa Hispania.

Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas alisema mechi hiyo ni sehemu ya uwajibikaji wa kampuni yao katika kuendeleza soka nchini.

Tarimba alisema walifanikisha kuileta Everton inayoshiriki Ligi Kuu ya England na kuleta msisimko wa soka  nchini  na ujio wa Sevilla ni mwendelezo wa majukumu yao katika maendeleo ya soka.

Kocha Mkuu wa Sevilla FC, Joaquin Caparros ambaye jana ilikuwa mechi  yake ya mwisho baada ya kusitishiwa mkataba, alisema kuwa wanaichukulia mechi hiyo kwa ukubwa wake na hawategemei kufungwa.

 Caparros alisema kuwa wanafurahi kucheza na Simba ambayo imetwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya pili wakiwa bado hawajamaliza mechi za ligi.

“Ni moja ya mechi ambayo kwetu ni muhimu pamoja na kumaliza msimu wa ligi. Tuna furaha kucheza na Simba, lakini tunahitaji matokeo mazuri pamoja na kuwa mechi maalumu ya kirafiki,” alisema Caparros.

Alisema hawawezi kuidharau Simba katika mchezo huo ambao utachezeshwa na mwamuzi wa Fifa, Herry Sasii wa Dar es Salaam.

“Tumeambiwa  Simba ni timu bora wakati inacheza nyumbani na wapo kwa ajili ya kuvunja rekodi ya timu hiyo katika uwanja wake wa nyumbani,” alisema kocha huyo.

Nahodha wa timu hiyo, Jesus Navas alisema wamejiandaa vyema na wataonyesha mchezo mzuri dhidi ya wapinzani wao.

Pia mshambuliaji nyota wa Sevilla, Ben Yedder alisema wamejiandaa kikamilifu na mchezo huo na hali ya hewa si tatizo kwao.

Yedder ambaye anakumbuwa na mashabiki wa Manchester United baada ya kuwafunga mabao mawili na kuwatoa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita,  alisema wanajisikia fahari kucheza na Simba na ameahidi kucheza kwa kiwango bora mchezo huo.

Simba inacheza mchezo huo baada ya juzi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo ikiwa na mechi mbili mkononi dhidi ya Biashara United kabla ya kumaliza na Mtibwa Sugar.