Setien: Messi ana furaha Barcelona

Muktasari:

Kuna taarifa kwamba, ametibuana na baadhi ya mabosi ikidaiwa hafurahishwi na mambo yanavyokwenda hasa kubebeshwa lawama matokeo yanapokuwa mabaya.

Barcelona, Hispania. Hatima ya nahodha wa Barcelona, Lionel Messi kikosini humo bado ni kiza.

Kuna taarifa kwamba, ametibuana na baadhi ya mabosi ikidaiwa hafurahishwi na mambo yanavyokwenda hasa kubebeshwa lawama matokeo yanapokuwa mabaya.

Lakini kocha wake, Quique Setien amesema kuwa nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Argentina, ana furaha kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi.

Pia, amesema hajashtushwa na taarifa kwamba, Messi anajiandaa kuachana na klabu yake hiyo ya tangu utotoni mwishoni mwa msimu.

Messi (33), ambaye ameshinda mataji kibao akiwa na Barcelona na kushikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote, mkataba wake unafikia tamati Julai, 2021 na mpaka sasa hakujawa na mazungumzo ya kuongeza.

“Sijasikia lolote kutoka kwa Messi kuhusu kuondoka na sio jukumu langu kuchunguza taarifa hizo.” alisema.

Hivi karibuni, Messi alikaririwa akisema ni ndoto kwa Barcelona kubeba taji la Ulaya kwa mbinu za Setien.

Pia, alizozana hadharani Mkurugenzi wa Michezo wa Barcelona, Eric Abidal. Messi amekulia kwenye akademi ya Barcelona, La Masia na baadaye kupandishwa timu ya wakubwa.