Serikali yawaka kisa Amunike

Thursday July 11 2019

 

By Imani Makongoro

SIKU chache baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza kusitisha mkataba wa aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Emmanuel Amunike, serikali imeonekana kuchukizwa na kuliwakia shirikisho hilo kwa mambo yanayoendelea TFF.

Katika mahojiano na Mwanaspoti jana Jumatano, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema Serikali haipingi uamuzi wa TFF kuachana na Amunike, lakini uamuzi wao uwe na sababu na malengo ya kuendeleza soka.

“Ni halali kwa TFF kufanya uamuzi huo, lakini uamuzi wao uwe na sababu za msingi na malengo ya kuendeleza soka,” alisema Mwakyembe na kufafanua.

“Nasema hivyo kwa kuwa nina matumaini hawajafanya uamuzi huo kwa kuigiza Misri, na naamini katika kuigiza basi unaigiza kikamilifu, hivyo kama ni kuigiza Misri isingeishia kwa kocha, wangeendelea zaidi ya hapo na wao kujiuzulu,” alisema Mwakyembe.

Shirikisho la Soka la Misri lilitangaza kumtimua aliyekuwa Kocha wa timu yao, Janvier Aguirre saa chache baada ya wenyeji kutimuliwa kwenye Fainali za Afcon 2019 kwa kufungwa bao 1-0 na Bafana Bafana ya Afrika.

Rais wa shirikisho hilo la Misri, Hany Abou-Rida alitangaza kumtimua kocha huyo kabla na yeye kujiuzulu nafasi hiyo sambamba na baadhi ya viongozi wenzake, kabla ya Jumatatu TFF nayo kutangaza kusitisha mkataba Amunike kwa makubaliano ya pande mbili, ikiwa ni siku chache tangu serikali ilipokutana naye kueleza imani yao kwake.

Waziri Mwakyembe alisema kama uamuzi huo ni wa kuendeleza soka, basi serikali ilitegemea wangekuja na mpango mkakati wa kuitoa nchi hapa ilipo na kufika hatua nyingine.

“Japo najua ni vigumu TFF kubadilika na kuiona serikali kama mshirika wa michezo yote nchini, lakini kwa ishu ya Amunike, haikuwa busara serikali kupata taarifa za kuondolewa kwake kupitia vyombo vya habari.

“Wamekuwa wakija kwetu na serikali imekuwa na wajibu katika kuhudumia timu ya taifa, lakini leo hii kocha anaondolewa bila kuihusisha serikali?” Alihoji Mwakyembe.

Alisema anapigania ubora wa soka nchini na hiki ndio kipindi cha kuhakikisha soka la Tanzania linarudi katika mstari huku akibainisha kama ni Fifa wote wanakujua.

“Lazima soka linyooke na mfano mdogo tu ni, leo (jana) Jumatano niliitisha mkutano kati ya Wizara, TFF, Bodi ya Ligi, TRA, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Idara ya Kazi na Baraza la Michezo (BMT).

“Lengo lilikuwa kubadilishana mawazo kuhusu hatma ya soka la baada ya Stars kushindwa kuingia 16 Bora kwenye Afcon, kwani kabla nilikutana na Kocha Amunike ambaye alinipa picha itakayotusaidia,” alisema Mwakyembe.

Alisema baada ya kikao na Amunike ilikuwa akutane na Waandishi wa Habari za Michezo kwani Wizara haijawahi kukaa nao ili kujadili mustakabali wa soka nchini na baada ya hapo ilikuwa TFF jana Jumatano.

“Siku niliyopanga kukutana na waandishi wa michezo TFF nao waliitisha mkutano, nikaahirisha, ajabu leo (jana) katika mkutano wangu wamekuja wote isipokuwa watu wa TFF na Bodi ya Ligi, nimeiagiza BMT iwapate taarifa nikutane nao Julai 24,” alisema.

Alisema Tanzania haiwezi kuwa nchi ya kutegemea kumuomba Mungu ili wafanye vizuri kwenye soka huku akihoji kwani timu tunazoshindana nazo hazina Mungu?

Hata hivyo, Rais wa TFF, Wallace Karia alipoulizwa kuhusu taarifa hiyo ya waziri alisema hawezi kujibu lolote kwa kuwa aliyezungumza ni waziri.

“Waziri amekwishazungumza, nitasema nini? Alihoji Karia na kueleza TFF haijawahi kuacha kuhudhuria mkutano wa waziri kila inapobidi na mkutano wa leo haujui ni kitu gani kimetokea.

“Niko safarini Rwanda, lakini sikuwa na taarifa hiyo ya kikao cha waziri na kama nilivyokwishasema TFF haiacha kukutana na waziri anapotuhitaji, hatuwezi kufanya hivyo, labda kutakuwa na kitu tu kimetokea katikati, ila hatuwezi,” alisisitiza.

Advertisement