Serikali yaruhusu nyota 10 wa kigeni kama kawaida

Muktasari:

Moja ya vigezo vya mchezaji wa kigeni anayetakiwa kusajiliwa na klabu za Ligi Kuu ni awe mchezaji wa timu ya Taifa katika nchi anakotoka pia awe mchezaji wa Ligi Kuu.

SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imebariki klabu za Ligi Kuu Bara kuendelea kusajili wachezaji 10 wa kigeni kutokana na wadau wengi kutaka iwe hivyo.

Hata hivyo Mwakyembe amezitaka klabu kufanya usajili wa wachezaji wenye viwango na si bora wachezaji.

"Klabu zetu hivi sasa ziko katika hekaheka za usajiliwa wachezaji wanaowataka kwa ajili ya msimu ujao.

"Nawatakia kila la kheri katika  usajili wao lakini mlete vifaa vya kuwafaa sio vifaa vya kuwavaa na kuwavuruga mkaishia kuvutana kwa malumbano yasiyo na tija kwenye mitandao na mikutano yenu badala ya kucheza soka" amesema Mwakyembe.

Mwakyembe amesema kutokana na mjadala waliouendesha wameona idadi ya wachezaji wa kigeni kwenye ligi hiyo ibaki 10 kama ilivyokuwa awali

"Kulikuwa na mjadala niliouanzisha kuhusu idadi ya wachezaji wa nje kwenye ligi zetu sio kwa soka tu ila na michezo mingine.

"Utata ulizuka mwaka juzi niliupata kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na ulitokea Arusha baada ya ushindi wa timu moja sitaitaja jina lakini timu hiyo ilikuwa na wachezaji karibu wote kutoka Uganda na wakati ni ya Tanzania.

"Katika mjadala huu tumepata muitikio mzuri sana na tumepata kupitia mijadala ya ana kwa ana na mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Instagram na barua pepe," amesema

Mwakyembe amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na wachezaji na wataalamu wa soka kutoka nje kwani wanaleta chachu katika maendeleo ya michezo kwa kuongeza ushindani na kuboresha viwango vya wachezaji wa Tanzania na ligi za ndani hivyo kuvutia wafadhili na

"Wadau  wa michezo wapatao 809 kati ya 977 sawa na asilimia 82.8 walipendekeza idadi ya wachezaji wa kigeni ibaki 10, wakati wadau 80 kati ya 977 walipendekeza usajili wa wachezaji wa kigeni usio na kikomo ili mradi klabu ina uwezo isajili tu.

"Wadau 64 sawa na asilimia sita walitaka idadi ya wachezaji wa kigeni iwe kati ya sita mpaka tisa na  wadu 24 kati ya asilimia 2.7 walipendekeza idadi isizidi watano" amesema Mwakyembe

Mwakyembe amesema suala la wachezaji wangapi wa kigeni wanatakiwa kucheza katika mchezo mmoja wanaiachia BMT ikae na wadau walijadili na kufikia muafaka.