Serikali yaipatia Stars Sh 7.2 milioni kuiua Ethiopia

Friday October 5 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi, Kenya. Kuelekea mechi ya kufuzu Kombe la Mabara Afrika, 2019 AFCON, Serikali kupitia wizara ya michezo imeipatia timu ya taifa Harambee Stars, Sh 7.2 milioni kwa ajili ya kugharamia safari ya kuelekea Ethiopia.

Harambee Stars inayohitaji ushindi wa lazima dhidi ya Ethiopia ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata tiketi ya kuelekea Cameroon mwakani, itaondoka nchini kesho kwa ajili ya mechi hiyo itakayopigwa Oktoba 10.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (FKF), Nick Mwendwa alisema mapema leo kuhusu ukata unaokabili FKF kwa sasa, bado sio kitu kulingana na fedha zinazohitajika kwa ajili ya uendeshaji wa timu.

Mwendwa, alisema kwa sasa FKF, inahitaji Sh25 milioni, kwa ajili ya kukamilisha malipo ya posho ya wachezaji na mshahara wa kocha pamoja na gharama za usafiri wa timu hivyo basi kiasi kilichotolewa na serikali bado hakitoshi.

Kwa mujibu wa Mwendwa mbali na mechi ya Ethiopia, bado wanaidai Serikali fedha za motisha na posho ya mechi iliyopita dhidi ya Ghana na kwamba kuna kila sababu ya Serikali kujitahidi kutimiza ahadi hiyo la sivyo ndoto za kwenda Cameroon zinaweza kuyeyuka.

 “Serikali imetuma Sh7.2 milioni. Hii haitoshi kitu ukilinganisha na gharama kubwa iliyopo kwa sasa. Tuliomba 25 milioni, hiyo ni kwa ajili ya mechi ya Ethiopia ugenini na nyumbani. Pia bado wachezaji hawajalipwa posho ya mechi dhidi ya Ghana,” alisema Mwendwa.

Advertisement