Sergio Aguero majanga tu

Muktasari:

  • Kocha, Guardiola alisema kwamba madaktari wa Man City walimwambia awe na tahadhali na Aguero kwa sababu tatizo linalomkabili linaweza kumweka nje ya uwanja hadi Januari mwakani.

MANCHESTER, ENGLAND.STRAIKA, Sergio Aguero anawapa presha Manchester City katika kipindi hiki wakikabiliwa na mechi kibao kwenye Ligi Kuu England.

Fowadi huyo wa Kiargentina aliwekwa nje ya uwanja wakati Man City ilipoichapa Bournemouth 3-1 Jumamosi iliyopita kutokana na kusukumbuliwa na maumivu ya misuli na kuna mashaka makubwa huenda asiwepo pia kikosi hicho cha Pep Guardiola kitakapowakabili Watford na Chelsea.

Kocha, Guardiola alisema kwamba madaktari wa Man City walimwambia awe na tahadhali na Aguero kwa sababu tatizo linalomkabili linaweza kumweka nje ya uwanja hadi Januari mwakani.

“Madaktari wameniambia ile Ijumaa kwamba Sergio hapaswi kucheza,” alisema Guardiola.

“Kwamba kama atacheza, basi anaweza kuwa nje ya uwanja kwa wiki nne hadi tano. Mambo yapo hivyo na mwezi huu mechi ni nyingi mno, hayupo vizuri.”

Kutokana na hilo, Aguero ameibua mashaka makubwa kama atakuwamo kwenye kikosi cha Man City kitakachokwenda huko Vicarage Road kumenyana na Watford leo Jumanne na kuna wasiwasi pia hata mchezo wa huko Stamford Bridge Jumamosi hii anaweza kukosa pia.

Gabriel Jesus alianzishwa dhidi ya Bournemouth na hakuweza kuliweka jina lake kwenye orodha ya wafungaji.

Jesus amefunga bao moja tu kwenye Ligi Kuu England msimu huu.