Serengeti yaleta kicheko Arachuga

Muktasari:

  • Serengeti Boys inafanya mazoezi yao viwanja vya Agakhan nje kidogo ya jiji la Arusha ambapo wametakiwa wadau wa soka kuhudhuria mazoezi hayo na kutoa sapoti.

ARUSHA.KITENDO cha timu ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kuweka kambi jijini hapa, imekuwa neema kwa Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA).

Kikosi hicho kimeweka kambi fupi kabla ya safari yao ya kuelekea Uturuki kwenye mashindano UEFA Assist ambayo Serengeti wamealikwa na pia ni maandalizi ya fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana yatakayofanyika Aprili mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa ARFA, Zakayo Mjema amesema hatua ya Shirikisho la soka nchini (TFF) kuchagua Mkoa wa Arusha kuwa kituo cha kambi hiyo ni fursa kwao kuutangaza mkoa lakini pia ni fursa kwa timu zinazoshiriki ligi kucheza nao mechi za kirafiki kupata mbinu za soka.

“Hii ni bahati kubwa kwetu na wale wadau wanaojua nini hasa maendeleo ya soka, hivyo hadi sasa tumezungumza na timu zinazoshiriki ligi kama Arusha United na AFC wanaoshiriki FDL, Mbuni ambao ni mabingwa wa mkoa waombe ratiba ya kocha wa timu hiyo kucheza mechi za kirafiki, itawasaidia kupata mbinu za soka kutokana na vijana waliocheza soka la kimataifa,” alisema Mjema

Serengeti Boys inafanya mazoezi yao viwanja vya Agakhan nje kidogo ya jiji la Arusha ambapo wametakiwa wadau wa soka kuhudhuria mazoezi hayo na kutoa sapoti.

“Wadau wa soka waone kama ni fursa nao kusapoti timu ya Taifa pia kuwaangalia mazoezi yao,” alisema Mjema.