Serengeti yaishika pabaya Nigeria,vita ya Kombe la Dunia Brazil inaanza leo

Muktasari:

Tumepata maandalizi mazuri na tuko tayari kuwakabili Nigeria. Sisi kama wachezaji hatuwahofii na tunejipanga vyema kupata ushindi dhidi yao.

ACHANA na mashamsham za ufunguzi wa Fainali za Afrika kwa Vijana U17, mashabiki wa soka wana hamu ya kuziona dakika 90 za mchezo wa kwanza wa timu yao ya taifa, Serengeti Boys dhidi ya Nigeria, lakini nje ya uwanja mipango hesabu zimekamilika kimbinu na kisaikolojia.
Ahadi nono kwa wachezaji iliyotolewa na mlezi wa Serengeti, Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi na mipango ya kiufundi ya benchi la ufundi la Serengeti Boys chini ya Oscar Mirambo ni wazi kwamba vinaiweka timu hiyo kwenye nafasi nzuri ya kupata ushindi kwenye mchezo huo muhimu wa kwanza kwenye mashindano hayo.
Licha ya wengi kuitazama Nigeria kama moja ya timu tishio kwenye mashindano hayo, Kocha Mirambo ameshtukia kuwa nguvu ya timu hiyo ipo kwa wachezaji wawili ambao kama watadhibitiwa vilivyo basi shughuli ya kuwamaliza vijana hao wa Nigeria itakuwa nyepesi.
"Nimepata nafasi ya kuwafuatilia na kuwafanyia tathmini Nigeria. Nilichogundua wamekuwa wakipendelea mfumo wa 4-3-3 na kuna mshambuliaji wao mmoja mwenye kasi ndiye wamekuwa wakimtumia kusaka mabao kwa kumpigia mipira mirefu anayoitumia kufunga na kuzalisha mabao kutokana na kasi yake.
"Amekuwa akiifanya hiyo kazi ya kumchezesha huyo mshambuliaji ni kiungo wao mmoja ambaye kama ukifanikiwa kumdhibiti basi kazi inakuwa imekwisha. Tumeshalifanyia kazi hilo na tumejipanga kwanza kuhakikisha huyo kiungo hapati mwanya wa kumchezesha huyo mshambuliaji wao lakini pia kumzima yeye mwenyewe kwani ukikamata hao, umeua nguvu yote ya Nigeria," alisema Mirambo.
Naye nahodha wa Serengeti, Abraham Morice alisema timu iko tayari kwa ajili ya mashindano hayo.
"Tumepata maandalizi mazuri na tuko tayari kuwakabili Nigeria. Sisi kama wachezaji hatuwahofii na tunejipanga vyema kupata ushindi dhidi yao.
Tunaamini utejeo wa mwenzetu Kelvin John umetupa hamasa na molali zaidi ya kufanya vizuri kwenye mashindano haya," alisema Abraham.

MZUKA WA MAGARI
Lakini wakati Serengeti wakijipanga kuhakikisha wanaimaliza Nigeria, maandalizi yao yamenogeshwa zaidi na ahadi ya kila mchezaji kupewa gari na Mzee Mengi iwapo watafanikiwa kumaliza kwenye nafasi mbili za juu kwenye mashindano hayo.
"Nina mradi wa magari, yapo tayari kwa hiyo nawaahidi kila mchezaji kumpatia gari. Nataka kuona siku ile mnashuka uwanjani, kila mmoja anaingia kwenye gari lake. Mnatakiwa kila mmoja wenu aanze kujifundisha kuendesha gari," alisema Mengi.
Mimi naamini tutafanya vizuri na kwenda Kombe la Dunia na tayari nimeshaweka oda ya hoteli ambayo nitafikia. Nataka kuona siku ile mnafika ndiye nitakayewapokea," alisema Mengi.
Mbali na ahadi ya gari, Mzee Mengi pia ameahidi kutoa Shilingi 5 milioni kwa mchezaji atakayefunga bao la kwanza kwenye mchezo wa leo.
"Bao la kwanza ni muhimu sana kwani naamini litapelekea muwafunge Nigeria mabao mengi hivyo mtu atakayefunga bao la kwanza nitampatia zawadi ya Shilingi 5 milioni," alisema.

WANAIJA WABISHI
Lakini kwa upande wa Nigeria, Kocha Manu Garba alitamba wataishangaza Tanzania leo licha ya kuwa wenyeji.
"Hatuna presha yoyote ya kucheza na timu mwenyeji. Tunajua mashabiki watakuwa wengi uwanjani lakini siku zote shabiki anapenda soka zuri hivyo tutahakikisha tunawavuta mashabiki wao watushangilie sisi," alisema Garba
Mbali na mchezo huo, leo pia kutakuwa na mchezo mwingine wa Kundi A kati ya Angola na Uganda kabla ya kesho mechi za Kundi B nazo kuchezwa katika mfululizo wa michuano hiyo ya Afrika.