Serengeti na Uganda ni Do or die

Muktasari:

  • Akizungumzia changamoto za kikosi chake zilizoonekana katika mchezo wa kwanza, alisema benchi la ufundi limekaa na kufanya marekebisho ambayo anaamini yatakuwa na msaada katika mchezo wao wa pili.

NI presha tupu katika mchezo wa pili wa Kundi A, timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ wanapokutana na Uganda leo Alhamis, Uwanja wa Taifa.

Timu zote zilipoteza michezo yao ya kwanza baada ya Tanzania kufungwa 4-5 na Nigeria na baadaye Uganda wakifungwa 1-0 na Angola.

Mchezo huu utakuwa wa kufa na kupona kwa timu zote kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ambayo yatawasogeza nafasi ya kushiriki katika Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Bazil.

Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo alisema kuelekea mchezo huo hana cha kupoteza zaidi ya kufanya kila linalowezekana kupata pointi tatu uwanjani.

“Mchezo utakua mgumu na tunatambua hilo kwasababu wenzetu nao walipoteza, lakini tunaamini kabisa kwamba tutatoka na pointi tatu na tukiwa kambini tumekuwa tukizungumza na vijana wetu kuwaambia kwamba matokeo tuliyopata tumeyaacha uwanjani na tufikirie mchezo wa pili ambao tunaweza kutoka na matokeo,” alisema.

Akizungumzia changamoto za kikosi chake zilizoonekana katika mchezo wa kwanza, alisema benchi la ufundi limekaa na kufanya marekebisho ambayo anaamini yatakuwa na msaada katika mchezo wao wa pili.

“ Kuanzia kwenye ushambuliaji mpaka kwa kipa kote tumeangalia upya kwa namna ya kukaba na kushambulia, mpira mpaka ufike kwa kipa lazima kutakuwa na makosa kwenye kiungo na sehemu zingine hivyo kote tumeanza kuangalia upya japokuwa muda ni mchache,” alisema.

Aliongeza kupitia mazoezi waliyofanya na kikosi chake, kutakuwa na mabadiliko ya mbinu katika mchezo wao dhidi ya Uganda.

Naye mshambuliaji wa Serengeti, Kelvin John alisema walianza vibaya lakini hawajakata tamaa. “Tumeanza tu vibaya kwenye mchezo wa kwanza, naamini kabisa tutafanya vizuri kwenye michezo ijayo, kasi yangu niliyoanza nayo nitaiendeleza na nitafunga,” alisema mshambuliaji huyo hatari katika kikosi cha Serengeti Boys.

Naye kocha wa Uganda, Samuel Kwasi alisema “Najua wenzetu watakuwa wapo 12, mashabiki watakuwa wengi lakini sisi hayo hatujui.”