Serengeti Boys yatoshana nguvu na Arusha Utd

Muktasari:

  • Serengeti wanacheza michezo ya kujipima nguvu jijini Arusha walipoweka kambi, kabla hawajatimka nchini Uturuki katika Mashindano ya Uefa Assist.

TIMU ya Taifa Tanzania chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imeweza kutoshana nguvu na timu ya Ligi Daraja la Kwanza, Arusha Utd baada ya kutoka sare 1-1 mchezo uliopigwa katika uwanja wa Sheikh Abeid Karume.

Katika mchezo huo goli la Serengeti Boys lilifungwan na Kelvin John huku goli la Arusha Utd likifungwa na Mshamu Said, mechi hii ni ya kirafiki kwaajili ya kukiweka fiti kikosi cha Serengeti ambacho kimeweka kambi jijini Arusha wakijiandaa kutimkia nchini Uturuki katika mashindano ya Uefa Assit yatakayoanza mwanzoni mwa mwezi Machi.

Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Milambo aliliambia Mwanaspoti amefurahishwa na matokeo ambayo wameyapata katika mchezo huo, kwasababu amecheza na timu ambayo imekamilika.

“Wachezaji wangu wamecheza soka zuri sana nimefurahishwa na kiwango ambacho wamekionyesha katika mchezo huu, naamini tutakuwa bora zaidi,” alisema.

Milambo aliongeza kwamba anaomba Mungu wachezaji wake waendelee kuwa na moyo wa kujitolea katika Taifa lao ili waweze kufanya vizuri katika mashindano wanayoshiriki.

“Naomba Mungu waendelee kuwa na afya bora, kwasababu naamini wakiwa na afya nzuri kila kitu kitaenda sawa katika mashindano tunayoshiriki,” alisema.

Serengeti watashuka tena dimbani Jumatatu kucheza mchezo wa kirafiki  na Polis Tz jijini Arusha.