Serengeti Boys kutesti mitambo Cosafa

Muktasari:

TIMU ya Taifa ya Vijana U17, Serengeti Boys imealikwa na kupangwa kundi la kifo katika fainali za Vijana U17 kwa nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (Coasafa), zitakazofanyika kati ya Desemba 6-16 nchini Botswana.

Gaborone, Botswana. Wenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana U17, Serengeti Boys imepangwa kundi moja na vigogo vya soka vya Ukanda wa Kusini mwa Afrika (COSAFA) katika michuano ya Vijana itakayofanyika nchini Botswana mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa jioni hii na Baraza la Vyama vya Soka la Nchi za Kusini mwa Afrika (Cosafa), michuano hiyo itachezwa kwenye jiji la Gaborone kati ya Desemba 6-16.

Tanzania itashiriki kama waalikwa na imepangwa Kundi B sambamba na watetezi wa taji hilo nchi ya Angola, Afrika Kusini na Malawi, huku Kundi A likiwa na Namibia, wenyeji Botswana, Zambia na Eswatini (zamani Swaziland).

Michuano hiyo pia itaenda sambamba na michuano ya soka la wanawake kwa Vijana U20 ambapo droo yao nayo ilitangazwa jana, ambapo itashirikisha nchi saba wakiwamo wenyeji Botswana.

Viwanja vitatuvimepangwa kutumika kwa fainali hizo za Cosafa ukiwamo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 8,000 wa UB, Jamal na Uwanja wa Taifa wa Gaborone.

Hizo zitakuwa fainali muhimu kwa Serengeti Boys ambao wanatarajiwa kuwa wenyeji wa Fainali za Afrika kwa Vijana U17, Afcon 2019 zitakazofanyika Aprili mwakani jijini Dar es Salaam.

Serengeti ndio Mabingwa wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ikibeba taji hilo mara mbili mfululizo mwaka jana na mwaka huu, huku wakiwa ni washindi wa tatu wa fainali za Afcon 2019 Kanda ya Cecafa zilizofanyika nchini hivi karibuni.

Makundi yalivyo kwa Vijana U17;

Kundi A: Botswana, Zambia, Eswatini na Namibia

Kundi B: Angola, Tanzania, Malawi na Afrika Kusini

Kwa timu za Wanawake U20 ni;

Kundi A: Botswana, Zimbabwe, Malawi, Lesotho

Kundi B: Afrika Kusini, Namibia, Eswatini