Serengeti Boys inajipanga haswa

Muktasari:

Katika mazoezi ya Serengeti Boys mambo makubwa yaliyokuwa yakisisitizwa ni umakini wa kutupia mabao nyavuni.

Dar es Salaam. Kikosi cha Serengeti Boys kimendelea na mazoezi katika Uwanja wa JK Youth Park jijini Dar es Salaam kujiandaa na  fainali ya mashindano ya Afrika (AFCON) yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Aprili mwaka huu.


Katika mazoezi ya asubuhi leo Jumatano Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo aliwataka wachezaji wake wawe haraka katika kufanya mashambulia na kupata mabao kwa wingi.


Mirambo alikuwa akiwasisitiza viungo wake akiwemo, Maurice Abraham pamoja na mshambuliaji wake, Kelvin John wakipata mpira macho yao yaangalie goli kwani ndiyo njia pekee ya kufanikiwa katika kazi yao ya kutafuta mabao.


Vijana wa Serengeti Boys hawakuwa nyuma kwani walionekana kulimudu vizuri zoezi hilo. Viungo walipiga mipira mbele kwa wingi na washambuliaji walihakikisha wanafunga.

Mshambuliaji, Kelvin John alionekana kutisha katika kufunga kwani alipokuwa anaingia ndani ya 18, hakuwa na mambo mengi zaidi ya kufunga.


Serengeti Boys wanakabaliwa na Mashindano ya AFCON chini ya miaka 17, yanayotarajia kuanza Aprili nchini.