Serengeti Boys yafutiwa mechi

Friday March 15 2019

 

By CHARLES ABEL

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania, limefuta rasmi ziara ya timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 'Serengeti Boys' nchini Rwanda kwa ajili ya kushiriki mashindano maalum ya kirafiki kabla ya kuanza kwa mashindano ya soka ya Afrika kwa vijana wa umri huo Aprili 14 hadi 28 hapa nchini. 
Kufutwa kwa ziara hiyo kunalenga kuipa nafasi Serengeti Boys ya kwenda kufanya maandalizi katika moja ya vituo vya soka vya klabu maarufu za soka duniani ambayo yatafanyika kwa kipindi kisichopungua wiki tatu.
Rais wa TFF, Wallace Karia aliliambia gazeti hili kuwa shirikisho kwa kushirikiana na mlezi wa timu hiyo, Mzee Reginald Mengi wamepanga Serengeti Boys ikafanyie maandalizi yake Ulaya na sio Rwanda kutokana na uwepo wa miundombinu na wataalamu wa kutosha watakaoweza kurekebisha udhaifu wa timu kabla ya mashindano hayo.
"Baada ya mashindano ambayo tulialikwa kule Uturuki, kuna udhaifu ambao umebainika kwa timu na unatakiwa ufanyiwe kazi hivyo tumeamua tusiende Rwanda na badala yake tutaipeleka Serengeti Boys Ulaya katika mojawapo ya vituo vya soka vya timu kubwa kule.
Ikiwa huko itakuwa chini ya wakufunzi na makocha wa daraja la juu ambao wataitayarisha vyema timu ili hadi mashindano yatakapoanza, tuwe na timu imara ambayo itaweza kutwaa ubingwa na kufuzu Kombe la Dunia," alisema Karia.
Katika mashindano hayo ya mualiko yaliyofanyika Uturuki chini ya usimamizi na uratibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), Serengeti Boys iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 huku ikipoteza mechi mbili ambazo ni dhidi ya Guinea ilipochapwa mabao 2-1 na dhidi ya Uturuki ambapo ilitandikwa 5-0.

Advertisement