Senzo tatizo lake na tatizo la mpira wetu

Muktasari:

PETER KENYON Aliwahi kuwa mtendaji mkuu wa Man United akasepa na kutua Chelsea na maisha kuendelea kama kawa...

UJIO wa Senzo Mbatha Mazingisa kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa mabingwa wa Tanzania, Simba, ulielezwa kama mwanzo wa safari ya timu hiyo pendwa kuwa moja ya vilabu vikubwa barani Afrika.

Senzo alikuja kuchukua nafasi ya Crescentius Magori; mmoja wa viongozi wazoefu wa soka la Tanzania lakini pia akiwa na historia ya kuwa mmoja wa maofisa wa juu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Kwa hiyo, hata wakati anakuja, Simba tayari ilikuwa inaongozwa na mtu aliyekuwa anajua nini maana ya kuongoza taasisi kubwa. Tofauti pekee baina yao ilikuwa kwamba, Senzo alionekana kama hatua kadhaa mbele ya Magori.

Alikuja nchini kutoka kwao Afrika Kusini akiwa na uzoefu wa kuongoza soka kwa takribani miaka 20. Uzoefu huo unajumuisha kuongoza klabu kama Orlando Pirates na Platnums Stars.

Viwango vya Orlando Pirates – The Buccaneers, ndiyo hasa mahali Simba ilipokuwa inaota kwenda. Kama ilivyo kwa Wekundu wa Msimbazi sasa; Orlando inamilikiwa na mmoja wa matajiri mashuhuri wa Afrika Kusini, Irvin Khoza, na ni klabu yenye mamilioni ya wafuasi.

Juzi, baada ya takribani mwaka mmoja tu wa kujiunga na Simba; Senzo amejiunga na watani wa jadi wa Wekundu wa Msimbazi – Yanga, katika tukio lililoshangaza na kushtusha wengi.

Hakuna aliyeliona hili likitokea. Katika takribani miaka zaidi ya 70 ya utani wa jadi wa vilabu hivi viwili, hakujawahi kutokea kwa mtu wa hadhi, cheo na majukumu kama ya Senzo kuhama kutoka klabu moja kwenda nyingine.

Tumefikaje hapa?

Ujio wa Senzo Tanzania unatokana moja kwa moja na mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo mara baada ya kuanza kumilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji.

Mabadiliko haya yameletwa pia na mabadiliko ya mifumo ya uendeshaji wa vilabu vya Tanzania kutokana na mwongozo wa CAF na FIFA vilivyovitaka vilabu kuwa na mifumo yenye wataalamu waajiriwa wa taaluma mbalimbali ili kufanya timu ziendeshwe kisasa.

Mwongozo huo ndiyo ulioleta vyeo kama Msemaji (Ofisa Habari), Wahasibu, Masoko, Katibu Mkuu (CEO) wa kuajiriwa na vyeo vingine vingi.

Kihistoria, viongozi wa vilabu wa Tanzania na nchi nyingi duniani walikuwa ni watu wa kuchaguliwa na wanachama. Mamlaka ya viongozi yalitoka kwa wanachama waliowachagua na kuwaweka madarakani.

Kwa sasa, ingawa bado kuna viongozi wa kuchaguliwa na wanachama, wataalamu waajiriwa, taratibu, wanaanza kuaminiwa na kupewa majukumu makubwa ambayo wasingeweza kuyapata katika miaka ya nyuma.

Senzo ni mmoja wa wafaidikaji wa mfumo huu mpya. Raia wa Afrika Kusini asingeweza kupata cheo cha aina yoyote Simba kwa mfumo wa zamani wa viongozi kuchaguliwa na wanachama.

Tatizo kubwa ambalo Senzo na watendaji wengine wa vilabu kwa sasa wanakumbana nalo ni kwamba, bado kuna viongozi ambao akili na mawazo yao yako miaka 20 nyuma. Wanaajiri wataalamu lakini akili na mawazo yao bado yako kwenye mfumo wa zamani.

Hakuna klabu ya Tanzania ambayo tatizo hili ni kubwa kuliko Simba.

Ukiangalia safu yote ya viongozi wa juu wa Simba, utabaini kwamba viongozi wenye mamlaka ya kufanya maamuzi, wengi wao walikuwa viongozi wa klabu hiyo kwa namna moja au nyingine miaka 20 iliyopita.

Mwina Kaduguda- Kaimu Mwenyekiti wa Simba, alikuwa kiongozi wa klabu hiyo miaka 20 iliyopita. Kassim Dewji alikuwepo, Magori alikuwepo, Salim Abdallah Mhene (Try Again) alikuwepo na wengine zaidi. Kassim na Kaduguda walikuwa sehemu ya uongozi rasmi, lakini wengine walikuwa kupitia kundi la Friends of Simba lililokuwa na nguvu na ushawishi mkubwa ndani ya klabu kongwe nchini.

Friends of Simba walikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Simba kwa kufanya mambo ya ndani na nje ya uwanja. Kuna watu ambao huwa hawaheshimu uwezo wa makocha, viongozi na wachezaji kwa sababu wao huwa wanajua ni kwa namna gani hufanikisha ushindi.

Kundi hili pia lina watu ambao mara zote hufikiri kama washabiki zaidi kuliko viongozi. Ndiyo hao ambao mara nyingi utasikia wameingilia vikosi vinavyopangwa na makocha, kufukuza wachezaji na kuvunja mikataba na waajiriwa pale inapobidi.

Yanga wana matatizo yao. Lakini Frederick Mwakalebela, Dk. Mshindo Msolla ni watu wa mpira wa muda mrefu, lakini hawana mizizi Yanga kama ambayo Friends of Simba wanayo Msimbazi.

Azam wana matatizo yao tofauti lakini ni klabu isiyo na figisu za kiwango cha viongozi wa Simba ama Yanga. Wekundu wa Msimbazi ni daraja tofauti, linapokuja suala la kuwa na viongozi wanaoamini kwamba, Simba ni ya kwao na wana uwezo wa kuingilia na kufanya chochote wakati wowote – kwa sababu ya historia yao na klabu inayorudi nyuma miongo miwili.

Kwa hiyo, siku ambayo Senzo alitua Dar es Salaam, alikuwa anatua katika klabu ambayo ni ngumu kwake kutekeleza dira na maono yake pengine kuliko klabu nyingine yoyote hapa nchini Lakini, labda hakujua hilo.

Mafanikio yake

Ndani ya klabu, Senzo anakubalika kama mtu aliyekuwa na viwango vya juu kama mtawala. Alifika kazini kwa wakati na inaelezwa kwamba, alikuwa mkweli na muwazi kwa watumishi wote wa Simba. Kama hataki kitu angesema na kama anakataa jambo; angetafuta namna ya kulisema kiungwana.

Kwa watu waliofanya kazi naye, wanakiri kwamba kama mtendaji mkuu, alikuwa na kiwango ambacho hakiwezi kufananishwa na mwingine katika miaka ya karibuni.

Hata hivyo, mfumo wa Simba una mizungu mingi. Ni mizungu hiyo ndiyo iliyosababisha aondoke pasi na kuliliwa na wengi zaidi ya watu kushtuka tu.

Washabiki wa mpira wa Tanzania wanahusudu watu wawili; wachezaji na makocha. Wanawajua wachezaji wazuri wakiwaona na wanamjua kocha mzuri wakimwona. Hawa ndiyo pekee ambao, wanaona kazi zao hadharani.

Simba ikitwaa ubingwa, itakuwa kwa sababu ya mabao ya Meddie Kagere na John Bocco. Itakuwa kwa sababu ya ujanja ujanja wa Clatous Chama na umahiri wa Luis Miquissone. Itakuwa kwa sababu ya uimara wa Serge Pascal Wawa, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein kwenye ngome.

Washabiki watajaa kwenye viwanja kwa sababu klabu inafanya vema uwanjani. Washabiki hawatajua kwamba watendaji wa klabu wanafanya kazi kubwa kuhakikisha timu ipo kwenye kiwango cha juu; kiafya, kisaikolojia na kimwili.

Ukiuliza leo shabiki wa kawaida wa Simba ni nini hasa Senzo ameleta Simba, hakuna shabiki ambaye atajibu hilo swali. Uwanjani, Simba ilitwaa makombe ya kutosha kabla ya ujio wake.

Suala la Uwanja wa Bunju lilishughulikiwa kabla ya ujio wake, wachezaji wote mahiri wa Simba kwa sasa walisajiliwa kabla yake, Simba Queens ilianza kutengenezwa kabla hajafika na kwenye soka la vijana Simba iliwahi kuwa na timu bora kabisa ya vijana kabla hajafika.

Yanga kutamfaa Senzo?

Si rahisi. Tatizo kubwa la Tanzania ni kwamba bado mifumo ya vilabu vikubwa haijawa tayari kupokea na kuhudumiwa na wakweli, wawazi na wanaojali taaluma zao. Mifumo bado iko teketeke sana na ndiyo kwanza inajengwa.

Kila ukiitazama Yanga, unaona mkanganyiko wa majukumu ya mwekezaji wake, GSM pamoja na viongozi wa kuchaguliwa na wanachama. Haijulikani kama Senzo ni chaguo la viongozi au GSM.

Kwa kuanzia tu, Yanga –kwa sasa, haina cheo cha CEO ambacho Senzo alikuwa nacho Simba. Uamuzi wa kumchukua unaonekana umefanyika kwa lengo la kupoza machungu ya kuporwa mchezaji wake, Benard Morrisson, kuliko hasa mkakati wa muda mrefu wa kuwa na mtu wa aina yake.

Kama ameletwa na GSM na siku mwekezaji huyo akaamua kuondoka zake Yanga, viongozi hawataweza kubaki naye kwa sababu si wao waliomwajiri.

Na Yanga pia, kama ilivyo Simba, kuna watu wanaamini kwamba hakuna mgeni anayeyajua maslahi mapana ya klabu hiyo kuliko wazawa. Ipo siku ataambiwa; “Sawa bwana, wewe ni mtaalamu wetu lakini katika hili, tunaomba utupishe kidogo. Hili ni jambo letu”.

Bado tuna safari ndefu.