HISIA ZANGU: Senzo anaweza kuwa muhimu kuliko Chama

CLATOUS Chotta Chama ana mkataba na Simba lakini sijui zilitoka wapi habari za kwamba Chama angeweza kutangazwa mchezaji wa Yanga juzi. Na uvumi huu ulikuja huku ikijulikana wazi kwamba Simba hawawezi kuwauzia Yanga mchezaji kama Chama.

Habari ilivuruga vichwa vya watu wa Simba na wakaanza kuhaha mitandaoni. Yanga walionekana wana jambo lao la siri zito ambalo lingekuwa kama kisasi kwa Simba ambayo Jumamosi mchana walimtangaza staa wao, Bernard Morrison kuwa staa wao mpya.

Wakati watu wa Yanga wakiwa wameganda katika simu zao wakisubiri labda angetangazwa Chama, au John Bocco, au Meddie Kagere, au Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ghafla wakatangaziwa kuwasili kwa Bosi Mtendaji wa Simba, Senzo Mbatha Mazingisa.

Senzo amekuwa Simba tangu Septemba 7 mwaka jana akiwasili nchini kutokea Afrika Kusini na nafasi yake ilionekana kuhitajika mtu mwenye weledi mkubwa katika masuala ya soka. Nasikia alikuwa akiitendea haki nafasi yake Msimbazi.

Yanga hawakujua kama iliwapaswa kufurahia au kuhuzunika. Vyovyote ilivyo wangependa awe mchezaji staa lakini baada ya kustukia kwamba amekuwa bosi mtendaji wa Simba wakalazimika tu kufurahia ili mradi wamerudisha bomu la nyuklia Msimbazi.

Uhamisho wa Senzo kwenda Yanga una maana gani? Ni kitu kizuri kwao kama wameona kuna umuhimu wa kuwa na mtu kama Senzo. Mpaka sasa Yanga hawana nafasi ya CEO katika katiba yao ya sasa. Sijui Senzo amekwenda kama nani.

Nafasi ya Katibu Mkuu inahitaji mtu baada ya kuondoka kwa Katibu Mkuu aliyepita lakini kwa Senzo inaonekana nafasi sahihi zaidi kwake ni ile ya kuwa CEO. Kwa namna hii Senzo analazimika kwanza kushirikiana na watu wa Yanga katika mchakato mzima wa mabadiliko.

Mbele ya safari anaweza kuikuta nafasi yake ile ile aliyoiacha Simba kikatiba kama Yanga wataweza kupitisha mabadiliko. Akiwa na Simba tayari alishakuta mabadiliko na ndio maana ilikuwa rahisi kukuta cheo chake.

Kwa Yanga Senzo anaanzia chini zaidi. Anaanzia katika mchakato wenyewe wa mabadiliko. Hapa anakuwa na umuhimu mkubwa kwa sababu atakuwa kiunganishi kizuri kati ya Yanga na watu wa La Liga ambao wanaipa Yanga funzo la kuelekea katika mabadiliko.

Mtu kama Senzo ana uweledi katika kazi yake akiwa na uzoefu pia kutoka katika klabu za Platinum Stars na Orland Pirates ambazo amewahi kuzihudumu kwa nyakati tofauti. Kama vile haitoshi, muda wake aliokaa Simba umempa nafasi nzuri ya kujua kinachotakiwa katika soka la Tanzania.

Wakati baadhi ya mashabiki wa Yanga wakiinamisha vichwa chini kwa kutotangaziwa ujio wa mchezaji kama Chama, wanapaswa kuelewa kwamba watu kama Senzo ndio ambao sasa watalazimika kutengeneza mifumo imara ndani ya klabu ya Yanga kwa ajili ya kuwanasa au kuwatengeneza wachezaji kama Chama.

Watu wachache walioshangilia ujio wa mtu kama Senzo pale Yanga ni wale ambao labda wanaelewa kwamba klabu zetu zina upungufu mkubwa wa kiuendeshaji. Hili ni tatizo kubwa kwa klabu zetu kwa miaka mingi.

Kama Senzo anaweza kuigeuza Yanga kuwa taasisi yenye hadhi basi hilo ni la msingi kwa Yanga kwa sasa kuliko kutangaziwa uhamisho wa Chama au Bocco. Wachezaji huja na kupita lakini mifumo imara huwa haipiti. Inahitajika muda wote.

Kwa wale mashabiki wa Simba wanaojaribu kuuliza kwa kebehi ‘Kwani Senzo anacheza?’ wanapaswa kuulizia umuhimu wa Senzo au mtu wa nafasi yake katika klabu kama Simba. Tatizo letu kubwa ni kwamba mashabiki wa soka letu wamezama zaidi katika soka linalochezwa na wanaume 22 uwanjani. Hawatazami nje ya hapo.

Wasichofahamu ni kwamba mpira una mambo mengi ya nje ya uwanja kabla ya timu kuingia uwanjani. Mpira una mambo mengi ya kiutawala ambayo yanapaswa kusimama imara kabla ya timu kuingia uwanjani.

‘Wizi’ ambao Yanga wameufanya kwa Simba unaonyesha kwamba labda tumeanza kupevuka kiakili na kujua umuhimu wa masuala ya menejimenti. Zamani isingewezekana kwa klabu moja kumuiba mtendaji wa klabu nyingine kama hivi.

Kitu cha kwanza ambacho kingetazamwa ni namna gani mhusika angeweza kupeleka unazi wake kutoka katika timu moja kwenda nyingine. Zamani baadhi ya watu wa Yanga wasingeafiki kwa kuamini kwamba Senzo tayari amekuwa mnazi wa Simba.

Walau siku hizi tunaona watu wa nafasi yake au makocha huwa wanahama kutoka katika timu moja pinzani na kwenda kwa timu nyingine pinzani. Kitu cha msingi ni kufuata weledi wa kazi yako (Professionalism).

Peter Kenyon alikuwa Mtendaji wa Manchester United kwa siku nyingi lakini Roman Abramovich alilazimika kumpa ofa ya kuwa mtendaji wa klabu wake. Lilikuwa suala la maslahi na Professionalism ya hali ya juu. Ivan Gazidis wa Arsenal kwa sasa ni Mtendaji Mkuu wa AC Milan.

Kama tumefikia huku basi sitashangaa sana kuona klabu hizi zikianza kuibiana madaktari au maskauti kwa sababu ni mfumo wa kisasa usiojali zaidi unazi na badala yake unajikita zaidi katika kuiendesha klabu kiuweledi.

Kila la kheri kwa Senzo katika maisha yake mapya Jangwani lakini mashabiki wanazi wa Yanga wasidhani kwamba Senzo atakuwa akitoa siri za Simba kwa Yanga. Haitakuwa na maana yoyote kwa sababu kitu cha msingi kwa Yanga kwa sasa ni kujikita katika mabadiliko yao. Umbea kuhusu Simba sidhani kama utawasaidia sana wao katika kuiendesha klabu yao.

Sidhani kama kuna siri kubwa ndani ya Simba.