Senzo akabidhi ofisi, mbadala ajadiliwa

JANA Jumatatu jioni Agosti 10, 2020 aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alikabidhi ofisi na nyaraka za klabu hiyo.

Kabla ya kukabidhi nyaraka za waajiri wake wa zamani, Mshauri Mkuu wa Mwenyekiti wa Bodi, Crescetius Magori alisema Senzo tangu atangaze kujiuzulu alikuwa hapatikani hewani kwa maana ya kwamba simu zake za mkononi zilizimwa.

Hivyo kupitia taarifa hiyo, Magori alimtaka Senzo kwenda kukabidhi ofisi kama utaratibu wa kazi ulivyo sehemu yoyote ambayo mtu anaajiriwa.

Mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, ameiambia Mwanaspoti Online leo Jumanne Agosti 11, 2020 kuwa bosi huyo alitinga ofisini hapo jana jioni na kukabidhi kila kitu.

"Jana (Jumatatu) jioni alikabidhi ofisi kama utaratibu ulivyo wa kazi, ni kweli hakupatikana hewani na alikuja tu kwa kushitukiza, kikubwa ni hilo kukabidhi ili maisha mengine yaendelee," amesema

Kuhusu mbadala wake, kigogo huyo amesema; "Kuna kikao kinaendelea leo ambacho wanajadili nani atakaimu kwa wakati huu huku mchakato mwingine wa kutangaza ajira ukifuata hapo baadaye.

"Nafasi ya CEO ni ya kuajiriwa hivyo taratibu zote za ajira zinapaswa kufuatwa, ni lazima kutuliza akili kufanya hivyo, lakini mtu wa kukaimu atapatika na huenda akatangazwa hata leo hii hii," amesema

Imeelezwa kwamba mtu atakayepatikana kukaimu nafasi hiyo kutoka ndani ya kikao hicho hapaswi kutoka kwenye Bodi ya Wakurugenzi kwamba maana kuwa asiwe mjumbe wa bodi hiyo ambapo Magori ni miongoni mwa wanaotajwa kukaimu kiti hicho.