Senzo afichua kile kilichomtoa Simba ghafla- 1

KATIKA mambo yaliyowavuruga Yanga kwenye usajili wa dirisha kubwa lililopita ni uhamisho wa utata wa winga wao, Bernard Morrison, alipotimkia Simba, lakini nao waliamua kujibu mapigo kwa kumchukua Mtendaji Mkuu wao, Senzo Mazingisa na kuwa Mshauri Mkuu Jangwani

Simba walikereka kwani hawakutarajia kama Senzo, angeondoka kwao ghafla kipindi hiki, hasa baada ya kufanya kazi kubwa ya kuiwekea klabu yao misingi bora ya kiutendaji na kilichowauma zaidi ni kitendo cha kujiunga kwa wapinzani wao.

Kutua kwa Senzo ndani ya Yanga, kuliwapa faraja Yanga ambao licha ya kuahidi kwenda Fifa kumpigania Morrison, wakidai bado ni mchezaji wao mwenye mkataba wa miaka miwili, waliamini wamewapiga bao la maana Simba kwa kumpata bosi huyo raia wa Afrika Kusini kwa kutambua yeye ni ‘mastermind’ anayeweza kuwaleta klabu yao ya Yanga wachezaji bora zaidi ya Mghana huyo na pia kuifanyia makubwa klabu hiyo katika harakati zake ya kutaka iendeshwe kisasa.

Katika kuiunda upya Yanga, klabu hiyo katika dirisha lililopita imesajili wachezaji wengi kuliko klabu nyingine yoyote Ligi Kuu Bara pamoja na kuleta makocha wapya ambao CV zao zinatisha.

Mwanaspoti imefanya mahojiano maalum na Senzo na kigogo huyo amefunguka mambo mengi ikiwamo maamuzi yake ya kutoka Simba kujiunga Yanga na juu ya mipango yake Jangwani. Endelea naye...!

MAISHA MAPYA YAKOJE?

“Mimi ni profeshno nimekuja Yanga nimekutana na watu tofauti na wana utamaduni tofauti, siasa za mpira ni zilezile lakini soka ni soka hakuna kinachobadilika, kinachotofautisha ni jinsi kila klabu inavyofanya mambo yake ila imekuwa changamoto nzuri kwangu.

“Nafurahia maisha ya hapa sasa, kuna majukumu mengi ya kufanya na kitu muhimu ni kuwa bize na majukumu yangu ili kila kitu ninachotakiwa kifanyike kiwe sawa,” anasema Senzo.

“Nafikiri watu wanatakiwa kuelewa juu ya uamuzi wangu wa kutoka Simba na kuja Yanga, nakumbuka tayari kwenye akili yangu kulikuwa na uamuzi wa kuondoka Msimbazi, ilikuwa ni kama mwezi nyuma kabla ya kuhama kwangu, nakumbuka nilikuwa nataka kuondoka Tanzania na akili kubwa ilikuwa kurudi Afrika Kusini kwani sikuona uwezekano wa haraka kama naweza kuja kufanya kazi katika klabu nyingine.

“Baada ya kama mwezi mmoja kuna mambo yakaanza kujitokeza, hapo ndipo uamuzi wa kuja Yanga ukaanza kujionyesha, niliona kuna klabu inataka kwenda katika mafanikio ambayo tunaweza kupita kwa pamoja na hapo ndio uamuzi wa kuja Yanga ukaanza, ila haikuwa kabisa eti natoka klabu hii kisha nakwenda nyingine na kikubwa kingine nilikuwa bado nina mapenzi mazuri na nchi hii, pia niliona bado sijatumika vizuri katika kufanya kazi kwangu hapa Tanzania,” anasema Senzo na kuongeza; “Sio yote, yapo ambayo nimefanikiwa, ila kuna mambo kama klabu kujitengeneza vyema na kuvuna pesa hili niliona bado halijakamilika kwa muda ambao nimeishi hapa Tanzania kwa kiasi ambacho naweza kusema hapa nimekamilisha hili kwa uhakika.”

“Unajua hii ni changamoto kubwa kwangu, unatoka kwenye klabu ambayo umeifanyia mambo mazuri ukiisaidia kuchukua mataji mawili makubwa na ngao na kuna mengine makubwa umeyafanya, umeifanya klabu kujiweka katika ramani nzuri ya kutambulika kibiashara lakini sasa nakwenda kwenye klabu ambayo haijachukua taji lolote ndani ya miaka mitatu kubwa naona kiu ya viongozi wakubwa wa klabu wakitamani kuona mambo yanabadilika na kuwa klabu kubwa mazingira kama haya nikaona kuna haja ya kuungana nao katika mabadiliko ya namna hiyo.

“Kwa wakati huo sikuona kama itakuja kuwa suala kubwa na gumu ambalo litashtua watu mpaka lilipotokea ndio nikaona kumbe nimefanya uamuzi mgumu, binafsi niliona akili yangu inaniambia mimi ni mweledi naweza kwenda kufanya kazi sehemu yoyote pia natakiwa kuwaheshimu waajiri wangu waliopita (Simba) kwa kuwaheshimu kwa kunipa nafasi ya kuja Tanzania, nawashukuru kwa kunipa hiyo nafasi lakini pia kwa kuniruhusu kufanya kazi zangu.

HUKUKABIDHI OFISI SIMBA?

“Nimeweka ahadi kwamba sitazungumzia kwa sasa mambo yaliyopita na waajiri wangu waliopita, kitu ambacho naweza kusema ni kwamba nimeondoka Simba nikiwa nimekamilisha kuwakabidhi vitu vyote vya msingi ambavyo nilitakiwa kuvikabidhi, unajua nilijua kutakuja kutokea mambo kama haya, muhimu walijua kwamba nitaondoka, nilishafanya uamuzi na niliwajulisha watu muhimu ambao walipaswa kujua hilo.

“Kitu ambacho naweza kuwaambia ni kwamba wakati natangaza kwamba naondoka ndani ya klabu ya Simba kwa jamii nzima, nakumbuka ilikuwa Jumapili, siku iliyofuata Jumatatu mchana nilikwenda kwenye ofisi kukabidhi funguo za gari, funguo za ofisi lakini pia nilitaka kuwakabidhi baadhi ya mafaili na vitu vingine lakini nikashangaa nikawakuta watu ndani ya ofisi yangu ambao baadhi ni wajumbe wa bodi ya klabu sasa ndio maana nasema sioni sababu ya kuliongelea hili.

“Nilipo-kutana nao walikuwa na maswali mbalimbali walitaka baadhi ya vitu ambavyo hatukuwa tumekubaliana kabla ndio maana nakwambia mimi ni mweledi nimekuja Yanga kama mtu mweledi nitafanya kazi zangu na Yanga, lolote lililotokea au nililolifanya na waajiri wangu waliopita ni nafasi yangu kuyatumia hayo katika kuongeza uzoefu katika kazi yangu lakini hizi taarifa za kwamba naweza kuchukua vitu kutoka klabu fulani na kuja kuvitumia hapa Yanga mimi sio mtu mbaya kama hivyo.

“Sikuja hapa Tanzania nijenge nyumba wala kuja kuoa mwanamke mwingine na kukaa hapa moja kwa moja nimekuja hapa kufanya kazi kama mtu mwenye weledi, watu wanasahau mimi ni raia wa kigeni hapa, nataka kufanya kazi karibu muda wote sina muda wa kufanya mambo ambayo hayana faida kwangu.

“Ninachoweza kuwaambia Simba ni kwamba nawatakia kila la kheri, misimu miwili iliyopita tulikuwa pamoja tulishirikiana kutengeneza kikosi kwa pamoja kuna idadi ya mambo mazuri ambayo watayachukua na kuyatumia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na nawatakia kheri na wanajua kwamba nilikuwa sehemu ya hayo mazuri na huwezi kuyaondoa hayo mbali nami iwe unapenda au hupendi na naamini wanaweza kufanikiwa hata kama sipo pale, inawezekana kuna watu wanasahau hili, katika watu wote ambao wapo Simba hakuna aliyekuwepo wakati klabu ile inaanzishwa lakini mpaka sasa klabu ipo kwahiyo sisi wengine tunapita na hizi taasisi zitabaki.

ULIFANIKIWA WAPI?

“Wakati nafika nilikuta klabu inafanya vizuri lakini tuliifanya ikawa inafanya vizuri zaidi, tulifanya akili yetu kufikiria makubwa zaidi tulitengeneza utulivu wa watu kuiunga mkono klabu zaidi, tulirudisha uwajibikaji wenye weledi kwa sekretarieti na uongozi kwa ujumla na hapo maeneo ambayo tulifanikiwa na mengine hatukuweza, sidhani pia kama natakiwa kukwambia mimi ndiye niliyesimamia Simba ikawa na ofisi zake pale jengo la Diamond Plaza ingawa nilishirikiana na viongozi wengine.

“Tulitengeneza Simba kuwa katika uso wa watu kupata taarifa kwa kutengeneza tovuti na sura zingine za klabu ili watu kupata taarifa mbalimbali pia tulitengeneza mfumo mzuri wa kuwatambua wanachama na mashabiki wetu ili tuanze kutumia idadi yao kibiashara.

“Kifedha pia tulifanya vizuri kama klabu tulikuwa na bajeti ya kila kipindi na ninafurahi katika kipindi changu hatukuwahi kuwa nje ya matumizi kuzidi bajeti yetu, tulisajili wachezaji kulingana na kipato halisi tulichotarajia kukitumia. Uwanjani nako mambo yalijieleza, tulitwaa makombe matatu tulianza na Ngao ya Jamii, kisha Kombe la Shirikisho na ubingwa wa Ligi Kuu Bara,” anasema Senzo na kuongeza;

“Mwisho kabisa siwezi kusema ndani ya Simba sikupewa ushirikiano, nilipata wa kutosha hata kama kuna maeneo hatukushirikiana jambo la msingi tulifanikiwa kwa asilimia kubwa ya mipango tuliyojiwekea kipindi hicho.

NDANI YA YANGA

“Mipango yangu ndani ya Yanga ni rahisi sana. Tunatakiwa kwanza kurudisha klabu kuwa inayoendeshwa kwa weledi maeneo yote, tunatakiwa kutumia kwa faida idadi ya wanachama na mashabiki wanaoishabikia hii timu, klabu ijue inavuna kipi na mashabiki wajue wanaingiza kipi kwa mujibu wa katiba lakini pia katiba yenyewe ya klabu nayo iboreshwe na kuwa ya kisasa.

“Bahati nzuri tangu nimefika nimekuta watu wanapambana kubadilisha mfumo wa uendeshaji kitu ambacho ni hatua kubwa nimefurahi kuona viongozi wa klabu na wadhamini wanashirikiana kufanya kazi kubwa ya usiku na mchana kuhakikisha mchakato huu unamalizika kwa haraka na uwe na manufaa makubwa kwa klabu.

“Kubwa kuliko yote hayo ambalo ni kama linaloongoza ni kutaka kuona klabu inaanza kufanya vizuri uwanjani. Kama timu haifanyi vizuri hayo mengine yote yatakayobadilika hayatakuwa na faida. Lazima timu iwe inashinda kibabe uwanjani na hapo ndipo tutakapopata nafasi ya kufikiria mambo mazuri makubwa mengine nje ya uwanja kama kuongeza ufanisi katika miundo mbinu, uwajibikaji katika maofisi, pia kuhakikisha tunakuwa na uwanja wa mazoezi. Kwahiyo kubwa na muhimu kwangu ni kwamba Yanga tuwe na kikosi bora kitakachoweza kupambana na timu yoyote na tukashinda.

“Jambo la pili ni katika hili la mabadiliko ambalo viongozi waliahidi kabla sijaingia ndani yanakuwa na sura nzuri ambayo watu wa nje watasema ndio, hapa uongozi umetupeleka sehemu sahihi kitu muhimu kwangu sasa ni kushirikiana nao kwa kasi na kusaidia kuboresha maeneo ambayo nina uzoefu nayo na mwisho la tatu ni kusimamia kuweka mfumo mzuri wa kutambulika kwa wanachama wetu na mashabiki wetu kwa faida ya klabu kifedha, unajua huwezi kuendesha klabu hasa kubwa kama hii bila ya kuwa na kipato cha kutosha kinachoaminika.

Je, Unajua mambo manne makubwa aLIYOPANGA KUYAFANYA na uamuzi mgumu alioufanya Yanga? Usikose Mwanaspoti LA kesho Jumanne.