Senzo aanza kwa mabadiliko Yanga

Dar es Salaam. Uongozi wa Yanga umesema Senzo Mazingisa ameanza majukumu yake Yanga, kwa kufanya mambo matatu, kutengeneza mfumo wa uendeshaji, kusimamia kamati ya katiba na ile ya mabadiliko.

Senzo aliyewahi kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba kabla ya kutimkia Yanga wiki kadhaa zilizopita, ameajiriwa na mabingwa hao wa zamani kusaidia kusimamia mabadiliko ya utawala ndani ya klabu hiyo.

“Majukumu yake kwa sasa ni kuishauri klabu katika mchakato ambao tunaufanya na watu wa La Liga,” alisema Makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela.

Alisema tayari ameshiriki vikao vingi katika kushauri kuelekea kwenye mabadiliko ya uendeshaji wa klabu.

“Vingi vimefanyika tangu ameingia Yanga, lakini makubwa ni lile la kutengeneza mfumo wa uendeshaji, kusimamia kamati ya katiba na ya mabadiliko,” alisema Mwakalebela.

Awali, Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla alisema wapo kwenye mchakato wa kukamilisha andiko la kwanza la muundo mpya wa klabu hiyo.

“Kamati ya Sheria na Katiba italipitia kisha viongozi wa matawi nchi nzima watapelekewa na kutakuwa na kablasha la katiba pendekezo na muundo pendekezo.

“Tutatoa wiki tatu za majadiliano na kuvipitia kabla ya kwenda kwenye mkutano mkuu, ambao ajenda zitakuwa mbili, mabadiliko ya katiba na muundo wa uendeshaji wa klabu.

“Tukikamilisha mchakato wa mabadiliko, tunaachana na mambo ya katibu mkuu na mwenyekiti, tunaingia kwenye mfumo mpya,” alisema Dk Msolla