Senegal yashusha presha, Morocco freshi

Muktasari:

Suala la kupewa nafasi hatuliwekei maanani sana zaidi kilichopo mbele yetu ni kuhakikisha tunaonyesha kiwango kizuri ndani ya uwanja,” alisema Daf.

KATIKA kile kinachoonekana ni kutaka kupunguza presha kwa timu yake, kocha wa timu ya Taifa ya Senegal, Malick Daf amesema hadhani kama mashindano hayo yatakuwa rahisi kwa upande wao, licha ya kupewa nafasi kubwa kubeba ubingwa wa michuano hiyo ya Vijana U17.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari leo, Daf alisema kiuhalisia Senegal ina mlima mrefu wa kupanda katika fainali hizo tofauti na hisia za wengi.

“Soka limekuwa likibadilika kila wakati na naamini timu zimejiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano haya hivyo sidhani kama ni sahihi kusema sisi ndio tunapewa nafasi kubwa kutwaa ubingwa wa mashindano haya.

Suala la kupewa nafasi hatuliwekei maanani sana zaidi kilichopo mbele yetu ni kuhakikisha tunaonyesha kiwango kizuri ndani ya uwanja,” alisema Daf.

Kuhusu mechi ya kesho (leo) Jumatatu dhidi ya Morocco, kocha huyo alisema anaamini itakuwa ya ushindani kutokana na ubora wa wapinzani wao.

“Tumefanikiwa kuwaona Morocco kwenye mashindano ya kirafiki kule Uturuki. Ni timu nzuri na imara hivyo tunaamini mechi haitokuwa rahisi,” aliongeza Daf.

Katika kujibu mapigo Morocco kupitia Kocha Mkuu wake Jamal Sellan na nahodha wake, haiotan Abaida walisema wamekuja nchini kwa ajili ya kupambana na kwamba wanaamini watapata matokeo mazuri.