Sean ,Matty ndugu waliokamata kiungo cha Newcastle United EPL

Muktasari:

Sean ndiye aliyekuwa wa kwanza kung’ara katika timu ya vijana ya Newcastle, lakini Januari mwaka 2017 akapelekwa kwa mkopo katika klabu ya Kilmarnock inayoshiriki Ligi Kuu ya Scotland akiwa sambamba na makinda wenzake, Callum Roberts na Freddie Woodman.

NEWCASTLE, ENGLAND . WIKI iliyopita, mashabiki wa Ligi Kuu ya England walishuhudia Manchester United ikiumbuka mbele ya Newcastle United huku eneo la kiungo United wakitawaliwa vilivyo na ndugu wawili wa Newcastle, Sean na Matty Longstaff. Wakati Sean ni mkubwa, Matty ni mdogo na ndiye ambaye aliwaliza mashabiki wa United duniani kote baada ya kufunga bao zuri la nje ya boksi akimuacha David de Gea hana la kufanya. Wametokea wapi hawa ndugu wawili?

Mkubwa ni Sean David Longstaff ambaye alizaliwa Oktoba 30, 1997 katika eneo la Newcastle upon Tyne, England na ana umri wa miaka 21 wakati mdogo ni Matthew David Longstaff. Hata hivyo, Mathew anafahamika zaidi kwa jina la Matty. Matty alizaliwa Machi 21, 2000 na ana umri wa miaka 19.

Baba yao David Longstaff alikuwa mmoja kati ya wachezaji mahiri wa timu ya taifa ya England mchezo wa magongo ambapo alicheza mechi zaidi ya 100. Kwa sasa ni kocha wa timu ya Magongo ya Whitley Warriors. Baba yao anakiri kwamba watoto wake wamekuwa mashabiki wakubwa wa Newcastle tangu utotoni.

Sean ndiye aliyekuwa wa kwanza kung’ara katika timu ya vijana ya Newcastle, lakini Januari mwaka 2017 akapelekwa kwa mkopo katika klabu ya Kilmarnock inayoshiriki Ligi Kuu ya Scotland akiwa sambamba na makinda wenzake, Callum Roberts na Freddie Woodman.

Baada ya kumaliza kipindi chake cha mkopo na Kilmarnock, Sean alirudi katika kikosi cha Newcastle lakini akapelekwa tena kwa mkopo katika klabu ya daraja la pili ya Blackpool Julai 2017 kwa ajili ya kuendelea kukomazwa.

Mwishoni mwa msimu huo alirudi Newcastle na katika mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya kiwango chake kilimkosha kocha wa Newcastle wakati huo, Rafa Benitez ambaye aliamua kumpa mkataba wa miaka minne Novemba 2018.

Mechi yake ya kwanza katika kikosi cha wakubwa ilikuja Desemba 2018 wakati walipochapwa 4-0 na Liverpool akiingia kipindi cha pili. Wiki mbili baadaye alianza mechi yake ya kwanza katika pambano la FA kabla hajacheza mechi kamili ya Ligi Kuu dhidi ya Chelsea ugenini.

Alifunga bao lake la kwanza katika pambano la FA dhidi ya Blackburn Rovers kabla ya kucheza soka la kiwango cha juu katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Manchester City ambapo walishinda, huku akisababisha penalti ya bao la pili.

Februari 26, 2019, Sean aliifungia timu yake bao la kwanza katika ushindi wa mabao 2–0 dhidi ya Burnley. Hata hivyo, Machi 2019 aliumia vibaya goti lake na akakaa nje kwa mechi zote za msimu zilizobaki.

Kwa upande wa Matty, alijiunga katika shule ya soka ya Newcastle akiwa mtoto kama kaka yake. Baada ya kutesa katika soka la vijana kwa muda mrefu msimu huu amefanikiwa kutinga katika kikosi cha kwanza cha Newcastle.

Kabla ya pambano la wikiendi iliyopita mechi yake ya kwanza kwa Newcastle ilikuja katika pambano la kombe la Ligi dhidi ya Leicester City Agosti 28, 2019 ambapo alianza katika mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya 1-1 huku Leicester wakishinda kwa penalti 4-2.

Pambano lake la pili ni dhidi ya Manchester United ambalo lilikuwa lake la kwanza la ligi. Alifunga bao katika dakika ya 72 na kuhitimisha siku yake nzuri huku akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi. Tuzo ya mchezaji bora wa mechi alikabidhiwa na kaka yake, Sean.

Kwa kufunga bao hilo, Matty aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kuifungia Newcastle United katika Ligi Kuu ya England kwenye mechi yake ya kwanza. Alifunga bao hilo akiwa na miaka 19 na siku 199.

Mama yao awasifia

Mama yao, Sean na Matty, Michelle amewasifia watoto wake kwa kufikia hatua waliyofikia huku akidai kwamba watoto hao walikuwa wakigombana na kupendana kama ilivyo kwa watoto wengine pindi wakati wanakua. “Wapo karibu sana, wanapendana sana. Wakiwa watoto walikuwa wakipigana na kubishana, lakini siku zote wamekuwa wakisaidiana sana. Ni watu wazuri na hilo ni jambo muhimu sana,” anasema mama huyo.

“Ni watu wa kawaida, wazuri na wamebarikiwa kuwa na vipaji, lakini wamefanya kazi kubwa kufika walipofika. Kila mtu ‘shukrani nyingi kwako’ lakini mimi nasema sifa pia ziende kwao. Wote tunajivunia wao.”

Man United yamnyemelea kaka

Wakati Matty ndio kwanza alianza kutangaza jina lake wikiendi iliyopita, kaka yake tayari alionyesha makali msimu uliopita na inadaiwa kwamba kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amekuwa akimvizia staa huyo.

Mpaka sasa thamani yake inatajwa kuwa zaidi ya Pauni 40 milioni na mapema msimu huu, kocha wa Newcastle, Steve Bruce alimwambia Sean kupuuza uvumi wa kutakiwa na Manchester United na badala yake ajikite zaidi katika kuimarisha kiwango chake msimu huu ili kutengeneza jina lake katika ulimwengu wa soka. Nyota hao wamegeuka kuwa kivutio katika ligi hiyo kwa sasa.