Scholes amchana Ljungberg sio mtu wa kuivusha Arsenal

Tuesday December 3 2019

Scholes -amchana- Ljungberg - mtu - kuivusha -Arsenal-Asernal-kocha-Unai-Emery-mikoba-mwanasport-MwanaspotiSoka-MwanaspotiGazeti-

 

LONDON, ENGLAND. HAKUNA kocha yeyote duniani akapigiwa simu na kuambiwa kuna kazi ya kuinoa Arsenal kisha akakataa ofa hiyo. Hakuna.

Kwa kifupi kuwa kocha wa timu kama Arsenal ni heshima kubwa. Lakini, sasa Freddie Ljungberg amemtibua Paul Scholes na kumfanya amshambulie kwa maneno makali staa huyo wa zamani wa Arsenal baada ya kutajwa kuwa kocha mkuu wa muda huko Emirates.

Scholes, ambaye ni gwiji wa Manchester United amehoji uamuzi wa Ljungberg kushindwa kupigilia suti ya maana katika mechi yake ya kwanza kwenye kikosi cha Arsenal, kwa sababu hicho si kitu kinachoweza kutokea kirahisi rahisi tu.

Scholes amesema kwa Ljungberg kuamua kuvaa tu pajama la kijivu na fulana yenye shingo pana badala ya kutinga suti na tai, hiyo inaonyesha wazi yeye si mtu sahihi wa kuchukua mikoba ya Kocha Unai Emery.

Arsenal ilitoka 2-2 na Norwich City katika mechi yao ya kwanza tangu walipomfuta kazi aliyekuwa kocha wao Mhispaniola, Emery.

Scholes amemwambia Ljungberg aachane na mambo yake ya mitindo anapaswa kuwa makini na kiti anachokalia kwa sasa kama kweli anataka kuchaguliwa kuwa kocha wa kudumu kwenye timu hiyo. Utanashati ni kitu cha msingi kwenye timu zenye hadhi kubwa duniani kama ilivyo Arsenal.

Advertisement

“Ungemtarajia kumwona akiwa kwenye vazi la suti safi inayoendana na kazi yake kwa sasa. Mimi naona alianza vizuri kwa matokeo, lakini kuacha kuvaa suti na tai, huo ni ukosefu mkubwa wa nidhamu,” alisema Scholes na kuongeza.

“Sidhani kama yeye ni mtu sahihi kwenye kazi hiyo.”

Lakini, maneno hayo ya Scholes yanaweza kuwa kama kumpigia muziki tu mbuzi kwa sababu Ljungberg anachodai yeye hajioni kuwa ni kocha wa kudumu katika kikosi hicho cha Arsenal.

Sasa kitendo cha Kocha wa Leicester City, Brendan Rodgers kuwafungulia mlango Arsenal kama wanamtaka kinathibitisha wazi Ljungberg hatakuwa na muda mrefu wa kuendelea kukalia kiti cha ubosi huko kwenye kikosi hicho cha Emirates.

Ljungberg, ambaye alikuwamo kwenye kile kikosi cha Arsenal kilichocheza kwa msimu mzima bila ya kupoteza, alisema:

“Ni heshima kubwa. Nataka kufanya vizuri kwa kadri ninavyoweza kwenye klabu hii bora. Najisikia furaha na nataka nifanye kazi nzuri zaidi.

“Nipo hapa kuisaidia klabu kwa kadri niwezavyo, kurudisha ari klabuni na kwa mashabiki. Kama tutacheza soka zuri na kupata matokeo mazuri, hakutakuwa na kitu kingine cha kufanya kurudisha ari. Nina uhakika wa kufanya hilo, la sivyo singekubali kazi hii nilipoombwa kufanya hivyo.”

Scholes kisha akambebesha Shkodran Mustafi kuwa alihusika kwenye mabao yote mawili waliyofungwa Arsenal na kumpa kazi Pierre-Emerick Aubameyang kusawazisha kusaidia timu kupata sare.

Makocha kibao wamekuwa wakihusishwa na Arsenal baada ya kuachana na Emery na orodha hiyo inaoongozwa na Massimiliano Allegri, Nuno Espirito Santo, Mikel Arteta, Mauricio Pochettino na Brendan Rodgers.

Advertisement