Sasa tuwatengeneze kina Kagere wetu kuanzia chini

Muktasari:

  • Rackeem Shango licha ya umri wake mdogo, lakini ameamua kujiita Kagere na nguo zake anazovaa zinaandikwa namba 14 kama ishara ya kutambua kazi kubwa inayofanywa na Meddie Kagere straika wa Timu ya Simba kutoka Rwanda.

MAMA wa Rackeem Shango kutoka jijini Tanga anasema mtoto wake anapenda sana mpira, lakini kama mzazi hakuwa anajua kama mwanae ni shabiki lialia wa Simba mpaka alipomuona analia siku ile Simba ilipofungwa mabao 5-0 na AS Vita ya DR Congo.

Rackeem ni mtoto mwenye umri chini ya miaka 10, lakini ameonyesha anapenda sana soka sio tu kutazama watu wakicheza bali naye pia kuucheza na mara nyingi akitoka shule jambo analofanya ni kucheza mpira.

Katika maisha kuna watu ambao wanafanya jambo fulani baada ya kuvutiwa na mafanikio walioyapata watu wangine, hivyo uamua kuingia moja kwa moja kufanya vile wanavyofanya hao.

Kutokana na hali hiyo watu hufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo yao ya kuwa kama wale waliowatangulia ambao ndio huwa chachu ya wao kuja kufanikiwa.

Leo hii watu wengi wanamuona Mo Dewji kama shujaa wao katika mafanikio wanatamani siku moja nao waandikwe kwenye majarida makubwa kama forbes yakielezea utajiri wao. Leo kuna watu ni madaktari lakini ili kufikia hapo walivutiwa na kazi ya udaktari iliyokuwa ikifanywa na watu fulani ndipo na wao wakaamua kuingia kwenye hiyo fani.

Rackeem Shango licha ya umri wake mdogo, lakini ameamua kujiita Kagere na nguo zake anazovaa zinaandikwa namba 14 kama ishara ya kutambua kazi kubwa inayofanywa na Meddie Kagere straika wa Timu ya Simba kutoka Rwanda.

Kwanza nimpongeze huyu mtoto Rackeem kwa kuonyesha mapenzi makubwa kwa timu yake ya Simba lakini kubwa zaidi kukubali mafanikio ya Kagere anayetoka Afrika Mashariki, kwani angeweza kujiita hata Messi, Suarez, Ronaldo, Kun Aguero, Rashford, Lukaku, Hazard, Benzema, Mo Salah, Ozil, Mbappe, Pogba, Coutinho, Mane, Firmino na wakali wengine.

Kwa kifupi angeweza kujiita jina lolote la mchezaji mkubwa duniani, kama ambavyo baadhi ya nyota wa hapa nchini wamekuwa wakijibatiza majina ya mastaa wa kimataifa wanaotamba Ligi za Ulaya.

Ukimuangalia Rackeem unaweza ukasema huko mbeleni anaweza kuwa mcheza soka kwani hata umbo lake limekaa vizuri kiuchezaji, hivyo kama Simba ingeweza kuwekeza kwa mtoto huyo naamini wangeweza kumtengeneza Kagere wa miaka 12 ijayo. Lakini kwa utamaduni uliopo nchini, sio ajabu kuja kusikia mtoto huyo hayupo hata kwenye ramani ya mpira baada ya kumaliza masomo yake ya Sekondari kama Mungu atamjalia kufika huko.

Kagere ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi katika Ligi Kuu ya Tanzania na anafurahia maisha kuliko msomi wa shahada ya Biashara kutoka Chuo Cha Usimamizi wa Fedha anaefanya kazi benki. Hivyo maisha ya Rackeem yanaweza kuwa mazuri na yenye furaha iwapo kipaji chake kitaendelezwa.

Nimejaribu kuangalia picha moja ya Trent Alexander Arnold, beki wa kulia wa Liverpool wakati akiwa mdogo alipiga picha na Mr. Liverpool mwenyewe Nahodha Steven Gerrard enzi hizo. Kumbuka Gerrard alikuwa kiungo wa Liverpool na kwa taarifa yako hata Trent alianzia nafasi hiyo ya kiungo kabla ya kubadilisha na kucheza beki ya kulia na leo ni faida kwa Liverpool na timu ya Taifa ya England.

Trent anasema alikuwa akivutiwa na Gerrard enzi zake alipokuwa akicheza soka la kulipwa. Trent alichukuliwa na Academy ya Liverpool mwaka 2004 akiwa na miaka 6 kutoka Shule ya Msingi ya Kikatoliki ya Mtakatifu Mathew na kupewa nafasi ya kufanya majaribio mara tatu kwa wiki na baadae alichukuliwa moja kwa moja kujiunga na Academy hiyo chini ya kocha Ian Barrigan.

Liverpool waliweka kambi ya majira ya joto huko West Derby na Shule ya Trent ilipata mwaliko kushiriki kambi hiyo na Trent kuonyesha mapenzi makubwa kwa timu ya Liverpool na huo ndio ukawa mwanzo wa maisha yake ya soka. Wakati akiwa kwenye Academy aliendelea kufanya vizuri na hatimaye kupewa unahodha wa timu ya vijana ya Liverpool chini ya umri wa miaka 16. Mwaka 2015 Gerard alitoa ushauri kwa uongozi wa klabu hiyo kumpa thamani ya kudumu Trent Alexander-Arnold “TAA” kwani anaweza kuja kuwa msaada mkubwa kwao. Na mwaka 2016 Trent alipewa mkataba wa kudumu wa kuichezea Liverpool na sasa ndio tegemeo la timu hiyo na timu ya Taifa ya England upande wa kulia. Achana na Trent, kuna mtu anaitwa Harry Kane alizaliwa tarehe 28 Jully 1993 na kujiunga na Larkswood Primary Academy mpaka mwaka 2004 kisha kuhamia Chingford Foundation School akiwa hapo anakutana na jina la David Beckham kwamba naye alipita hapo. Hii ilimfanya Harry Kane kuona maisha ya mpira yanawezekana, hivyo akamfanya Beckham kuwa kiigizo chake (mafanikio ya David Beckham alimfanya Harry Kane kupenda mpira zaidi).

Itazameni timu ya vijana ya Nigeria U17 inayoshiriki fainali za AFCON U17 hapa Tanzania kikosi kizima cha Nigeria wachezaji wake wengi wanatokea kwenye Academy zilizo rasmi. Mfano, Shedrack Tanko (Ambassadors Academy), Suleman Shaibu (Hofafa FC), Sunday Steven (Abuja Football College), Clement Ikena (A & B Academy), Peter Agba (Falala Academy), Ibraheem Jabar (Olisa FC).

Hapa kwetu tunazo Academy zetu nyingi za kisiasa ambazo hazina faida kwa Taifa katika kutengeneza wachezaji wazuri kwa bahati mbaya zaidi ni kwamba vile vituo vyenye nia njema ya kuibua vipaji havina facilities za kutosha matokeo yake wanashindwa kutimiza malengo yao. Tuite wawekezaji waje.

Hapa ndipo tunapoona umuhimu wa klabu zetu au nchi kwa ujumla kuwa na Academy nyingi ambapo tungeweza kuwatengeneza kina Kagere wengi kupitia watoto wadogo kama hawa kina Rackeem Shango, ili baadaye waje kuwa msaada kwao na taifa kwa ujumla. Kila kitu kinawezekana buana!

Mo kama umeamua kuwekeza kwenye klabu ya Simba basi mtunze huyu Rackeem Shango na ipo siku utampata Kagere mzaliwa wa Tanga. Ningependa Manara amshauri Mo namna ya kumtunza na kumtengeneza Rackeem ili baadaye aje kuwa faida kwa Simba sio uishie kwenda Tanga kumbeba kifuani, kupiga picha na kupost Instagram tu. Katika soka hakuna njia ya mkato ila mipango mkakati tu!

Mwandishi amejitambulisha kama Msomaji wa Mwanaspoti kutoka Mwanza- 0716 605949.