Sarri presha tupu kisa ratiba ngumu

Muktasari:

  • Ratiba yao itahusisha pia fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Man City, Kombe la FA dhidi ya Manchester United na kwenda Ligi Kuu England ikimenyana na mahasimu wake wa London, Tottenham Hotspur na kuna mechi ugenini pia dhidi ya Malmo kwenye Europa League.

LONDON, ENGLAND.KOCHA Maurizio Sarri amefichua wasiwasi wa mastaa wake wa Chelsea huenda wakashindwa kumiliki ratiba ngumu inayowakabili katika kipindi hiki.

Chelsea jana Jumapili ilianza mchakamchaka wa kucheza mechi saba kali ndani ya siku 22 wakati ilipomenyana na Manchester City kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uwanjani Etihad.

Ratiba yao itahusisha pia fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Man City, Kombe la FA dhidi ya Manchester United na kwenda Ligi Kuu England ikimenyana na mahasimu wake wa London, Tottenham Hotspur na kuna mechi ugenini pia dhidi ya Malmo kwenye Europa League.

Alipoulizwa kama anaona ugumu wa kupambana na ratiba hiyo, Sarri alisema: “Hakika.

“Ni hasa, kama unapocheza mechi ngumu shughuli ni pevu, cheki unatakiwa kucheza mechi mbili dhidi ya Man City, moja dhidi ya Tottenham, moja dhidi ya Manchester United. Kisha kuna Europa League. Ni ngumu sana.”

Chelsea iliingia uwanjani jana kutafuta pointi za kuirudisha kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu England baada ya Man United kuiengua katika nafasi hiyo kufuatia ushindi wake wa mabao 3-0 dhidi ya Fulham huko uwanjani Craven Cottage juzi Jumamosi.

Nafasi ya nne inasakwa na timu kibao ikiwamo Man United, Arsenal na Chelsea yenyewe ili kukamatia nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Mechi ya jana Jumapili ilikuwa ngumu kwani Manchester City nayo ilikuwa ikihitaji ushindi ili kurudi kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiendelea kuchuana na Liverpool katika mbio za ubingwa wa ligi hiyo.