Sarri bado mechi moja tu afukuzwe kazi

Muktasari:

Sarri pia anakabiliwa na kesi nzito dhidi ya Tottenham Jumatano ijayo katika Ligi Kuu ya England. Ni ngumu kuona akiruka viunzi katika mechi hizi mbili dhidi ya Manchester City na Tottenham ambapo pambano moja linaweza kumnyima taji lake la kwanza katika maisha ya soka wakati pambano jingine linaweza kuhitimisha mbio zake za Top Four.

LONDON ,ENGLAND.NI kama kitabu kilichoandikwa na mwandishi wa zamani wa Tanzania, Hammie Rajab ‘Roho Mkononi’. Kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri ni kama vile anatembea na roho yake mkononi. Amebakiza kufungwa mechi moja tu atimuliwe.

Sarri na kikosi chake cha Chelsea leo Alhamisi wanatazamiwa kutinga uwanjani dhidi ya Malmo ya Sweden uwanjani Stamford Bridge katika pambano la Europa wakiongoza kwa matokeo ya mabao 2-1 ugenini wiki iliyopita lakini pambano hili halitaamua hatima yake.

Pambano la fainali Kombe la Ligi dhidi ya Manchester City dimba la Wembley wikiendi hii inayokuja inadaiwa ni la mwisho la Sarri Chelsea endapo atapokea kichapo kingine kutoka kwa City baada ya kuchapwa mabao 6-0 siku kumi zilizopita pale Etihad.

Jumatatu kazi ya Sarri ilikuwa imeshikiwa na kamba nyembamba baada ya Chelsea kutupwa nje ya Michuano ya FA na Manchester United ilipochapwa 2-0 huku mashabiki wakiimba kocha huyo alikuwa ameishiwa mbinu.

Juzi Sarri alikuwa mazoezini kama kawaida katika uwanja wa mazoezi Cobham lakini inadaiwa Bodi ya Chelsea imeandaa panga la kumuondoa endapo atapoteza pambano la wikiendi dhidi ya City ingawa wanafahamu ana nafasi kubwa ya kushinda mechi ya leo.

Mkurugenzi wa Chelsea, Mwanamama, Marina Granovskaia ambaye ana nguvu Chelsea alifanya kazi kubwa ya kuhakikisha Sarri anakuwa kocha wa Chelsea wakati wa dirisha la majira ya joto mwaka jana lakini kufuatia mazungumzo na vigogo wa Chelsea wamekubaliana mwisho wa Sarri umekaribia.

Sarri pia anakabiliwa na kesi nzito dhidi ya Tottenham Jumatano ijayo katika Ligi Kuu ya England. Ni ngumu kuona akiruka viunzi katika mechi hizi mbili dhidi ya Manchester City na Tottenham ambapo pambano moja linaweza kumnyima taji lake la kwanza katika maisha ya soka wakati pambano jingine linaweza kuhitimisha mbio zake za Top Four.

Kufuatia vichapo vitano katika mechi 10 ikiwemo vichapo vizito kutoka kwa Bournemouth na City, bodi ya Chelsea imepoteza imani na Sarri. Na sasa pia mashabiki wamepoteza imani na kocha huyo waliyemchukua kutoka Napoli.

Mashabiki wanaamini Sarri hana mbinu na amekuwa akivurunda pia katika wachezaji ambao anawaingiza uwanjani wakitokea benchi huku mfano mmoja ukiwa ule wa kumungiza uwanjani beki wa kulia, Davide Zappacosta katika pambano la United akichukua nafasi ya Cesar Azpilicueta.

Sarri alichukua uamuzi huo huku Chelsea ikiwa nyuma na wakati huohuo katika benchi kulikuwa na washambuliaji kama Callum Hudson-Odoi na Olivier Giroud. Mashabiki na wachambuzi wanashangwa pia na kitendo chake cha kumpanga Jorginho katika eneo la kiungo cha kati badala ya N’Golo Kante.

Kante anajulikana kama kiungo bora zaidi katika eneo la katikati hasa kiungo mkabaji lakini chini ya Sarri amekuwa akicheza kama kiungo wa kutoka nyuma kwenda mbele. Jorginho amekuwa akishutumiwa kwa kupiga pasi nyingi ambazo hazina madhara kwa adui.

Watu watatu wanatajwa kuwa wanaweza kupewa kazi ya muda endapo Sarri atafukuzwa anaweza kuwa Gianfranco Zola ambaye ni msaidizi wake. Kocha wa Ufundi, Eddie Newton pamoja na beki wa zamani wa Chelsea, Paulo Ferreira ambaye anafanya kazi na Newton.

Wakati hatima ya kocha wa Chelsea ikiwa njia panda, hatima ya klabu kwa ujumla nayo ipo njia panda baada ya tajiri wa klabu hiyo, Roman Abramovich huenda akaiuza timu hiyo baada ya kuwa katika mgogoro na Serikali ya Uingereza. Abramovich hajaonekana Stamford Bridge msimu huu baada ya Waingereza kumnyima viza ya kungia katika nchi hiyo. Chelsea pia huenda ikafungiwa na Fifa baada ya kudaiwa kusajili wachezaji 14 wa kigeni wenye chini ya umri wa miaka 18. Naye Eden Hazard akiwa katika hatihati huku ikielezwa anataka kujiunga na Real Madrid katika dirisha kubwa lijalo la majira ya joto.