Sarri ajutia kupangua kikosi Chelsea

Muktasari:

Kocha wa Chelsea Maurizio Sarri, amejilaumu kwa kupangua kikosi chake jambo lililosababisha kupoteza mchezo wa jana kwa kufungwa mabao 2-1 na timu inayoyumba katika Ligi Kuu England ya Wolverhampton Wanderers, kipigo kilichoishusha hadi nafasi ya nne katika msimamo.

London, England. Kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri amesema ameshtushwa na kipigo cha kushangaza walichokipata kutoka kwa Wolverhampton Wanderers jana Jumatano usiku huku akijilaumu kupangua kikosi.

Sarri ambaye wikiendi iliyopita alipata ushindi mbele ya mahasimu wao wa jiji la London, Fulham, aliidharau Wolves na kuwapumzisha nyota watano wa kikosi cha kwanza jambo lililoifanya Chelsea ifungwe mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Molineux.

Katika mchezo huo Chelsea ndiyo iliyoanza kupata bao la kuongoza katika dakika ya 18 likifungwa na Ruben Loftus-Cheek lakini ikashidnwa kuulinda uongozi huo na kuwaruhusu wenyeji kusawazisha na kupata bao la ushindi ndani ya dakika nne katika kipindi cha pili.

Kipigo hicho kimeishusha Chelsea hadi nafasi ya nne ikibaki na pointi 31 kumi nyuma ya vinara Manchester City ambao wataikaribisha Jumamosi hii kwenye dimba la Stamford Bridge.

Iwapo Chelsea itashindwa kuifunga Man City basi itakuwa imejiondoa rasmi katika mbio za kuwania nafasi nne za juu, baada ya wiki iliyopita Sarri kukiri kuwa timu yake imejiondoa katika mbio za ubingwa.

“Sisi hatutakuwa katika mbio za ubingwa lakini tutapigania kumaliza Ligi katika nafasi ya nne za juu,” alisema Sarri baada ya kufungwa mabao 3-1 na Tottenham.

Kocha huyo ambaye alisifiwa sana katika mechi za kwanza akiiwezesha Chelsea kucheza mechi 12 mfululizo bila kupoteza ukiwa ni msimu wake wa kwanza ndani ya klabu hiyo, hivi sasa anaonekana kuanza kupoteza mwelekeo na wengi wanamtabiria mabaya.

Sarri aliyetua Chelsea baada ya kutimuliwa kwa Antonio Conte mwishoni mwa msimu uliopita katika mechi za hivi karibuni amekuwa akilaumiwa kwa kumchezesha N’Golo Kante katika nafasi ya ulinzi badala ya kiungo ambako ameamua kumtumia Joginho.

“Kwa kweli nimeogopa sana sikutarajia kitu kama hichi tulianza vizuri lakini tukajitafutia matatizo kwa kushindwa kuzitumia nafasi tulizozitengeneza, tumepoteza nafasi nyingi na ikatugharimu,” alisema Sarri.

Alisema ni lazima wabadilike katika michezo ijayo ili waweze kurejesha hadhi yao, hata hivyo kocha huyo ameshindwa kuzungumza chochote kuhusu suala la usajili wa mwezi Januari.

&&&&