Sarpong apewa mbinu mbadala

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Yanga, Michaelo Sarpong ametakiwa kutuliza akili na kuangalia mikimbio yake upya kwa ajili ya kuifungia miamba hiyo ya soka nchini.

Sarpong alianza vizuri maisha yake ndani ya Yanga kwa kufunga katika mchezo wa kilele cha Wiki ya Mwananchi dhidi ya Eagle Noir ya Burundi wakati miamba hiyo ikiibuka na ushindi wa maboa 2-0.

Mshambuliaji huyo raia wa Ghana alifunga tena katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakati Yanga ikilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Baada ya hapo, mshambuliaji huyo hakufunga tena dhidi ya Mbeya City (0-0), Kagera Sugar (1-) na Mtibwa Sugar (1-0), licha ya kucheza katika michezo hiyo, ambayo wafungaji walikuwa Mukoko Tonombe na Lamine Moro.

Kocha wa Yanga, Zlatko Krmpotic alimtumia Sarpong katika mchezo wa juzi wa kirafiki dhidi ya KMKM uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, lakini pia hakufanikiwa kufunga licha ya kucheza kwa deakika 45 za kipindi cha pili.

Baada ya mchezo huo wa juzi usiku, Krmpotic alisema Sarpong anatakiwa kutuliza akili na kutoishi kwa dau la usajili lililotolewa kwa ajili yake, badala yake kuweka akili uwanjani na kukaa katika maeneo ya kufunga.

Kocha huyo raia wa Serbia alisenma mshambuliaji huyo ana uwezo mkubwa wa kucheza katika nafasi yake, lakini anatakiwa kuelekeza akili katika kufumania nyavu, suala ambalo ameshazungumza naye.

“Ni mchezaji mzuri na mwenye kila kitu cha mshambuliaji, suala la kutokuwa na mabao mengi hata mimi silifurahii kutokana na kutomaliza mechi mapema.

“Unapofunga mabao mengi unaimaliza mechi mapema, na suala la Sarpong nadhani ni la muda kidogo, anatakiwa kufikiria tu zaidi uwanjani na kuachana na gharama za usajili, kwasasabu anajua klabu na mashabiki.

“Naamini atabadilika na kuwa bora zaidi, tumezungumza na anajua sasa nini cha kufanya, kuanzia kwenye kukaa katika nafasi na mikimbio yake uwanjani kutoa nafasi,” alisema.