Sarpong, Dube, Morrison waongoza wapya Ligi Kuu waliong'ara

Tuesday September 15 2020

 

By Oliver Albert na Imani Makongoro

Dar es Salaam. Wakati Ligi Kuu Bara (VPL) ikiingia raundi ya tatu, baadhi ya wachezaji wapya wameonekana kung'ara tangu ligi hiyo ianze Septemba 6 wakiongozwa na Michael Sarpong wa Yanga na Prince Dube wa Azam.

Mpaka sasa KMC ndiyo inayoongoza ligi ikiwa na pointi sita sawa na Azam iliyo nafasi ya pili, Dodoma Jiji (nafasi ya tatu) na Biashara United iliyo katika nafasi ya nne.

Baadhi ya wachezaji wapya waliosajiliwa na klabu mbalimbali msimu huu wameng'ara katika mechi mbili walizocheza kwa kuzipa matokeo timu zao au kuhusika na matokeo waliyopata timu hizo.

Kwa upande wa Yanga, Michael Sarpong anawaongoza wenzie waliosajiliwa na kikosi hicho msimu huu kutokana aina yake ya uchezaji wa kasi, upambanaji na nguvu na mpaka sasa ameifungia timu hiyo bao moja lililoikoa kulala mbele ya Prisons katika mchezo wao wa kwanza uliofanyika Septemba 6 na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mchezaji huyo anaungana na wachezaji wengine wa Yanga waliong'ara katika mechi mbili ziliopita wakiwemo viungo Tuisila Kisinda na Mukoko Tunombe na Carlos Fernandes'Carlinho', mabeki Bakari Mwanyeto, Yassin Mustapha na Kibwana Shomari.

Kwa upnde wa mabingwa watetezi Simba, ni Benard Morrison pekee angalau aliyeng'ara kwa wachezaji wapya baada ya kucheza vizuri katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu dhdi ya Ihefu ambao Simba ilishinda mabao 2-1 lakini alipotezwa katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar uliofanyika Jumamosi iliyopita ambapo sehemu kubwa ya wachezaji wa timu hiyo hawakuwa katika ubora wao kutokana na kudhibitiwa vilivyo na wapinzani wao.

Advertisement

Wachezaji wengine waliong'ara katika mechi mbili zilizopita ni mashambuliaji wa Azam,Prince Dube ambaye ndio mgeni pekee anayeongoza katika chati ya ufungaji akiwa amefunga mabao mawili sawa na Hassan Kabunda wa KMC na Mzamiru Yassin wa  Simba.

Dube ameonekana kama akiendelea na kiwango hicho ataibeba sana Azam msimu huu kwani ni mchezaji mwenye kasi, mjanja ana asiyehofia mabeki wa timu pinzani.Ameiongoza Azam kushinda michezo yote miwili ya kwanza dhidi ya Polisi Tanzania alipotoa pasi ya bao lililofungwa na Obrey Chirwa na dhidi ya Coastal Union alipofunga mabao yote mawili yaliyowapa ushindi timu yake.

Pia mchezaji mwingine alinyeng'ara katika kikosi cha Azam ni kipa David Kissu ambaye ameidakia timu hiyo mechi zote mbili na hajaruhusu bao.

Kwa upande wa Namungo wachezaji kama Abdulharim Humud na Haruna Shamte wameng'ara kwa kucheza vizuri katika mechi zote mbili licha ya timu yao kushinda mechi moja dhidi ya Caostal Union kwa bao 1-0 na kupoteza dhidi ya Polisi Tanzania kwa bao 1-0.

Timu ngeni ya Dodoma Jiji Fc haikuwa nyuma katika usajili wa msimu huu ambao sasa umeanza kuwapa matunda kwani wachezaji wengi wapya wa kikosi hicho wamefanya vizuri katika mechi zao mbili zilizopita dhidi ya Mwadui waliyoshinda kwa bao 1-0 na JKT Tanzania waliyoshinda kwa mabao 2-0.

Mchezaji Dickson Ambundo waliyemsajili kutokea Gor Mahia amekuwa mmoja ya wachezaji wapya walioiba timu hiyo kwenye mechi mbili zilizopita.

Pia kuna wachezaji wengine kutoka KMC kama beki Andrew Vincent 'Dante' aliyesajiliwa akitokea Yanga ambaye ameonyesha kiwango kizuri na kuiongoza timu yake kushinda mechi zote mbili hivyo kuiongoza ligi.  

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema wachezaji wengi wanaocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu wameanza vizuri.

"Hivi sasa makocha wamewaachia wachezaji kucheza mchezo wa wazi na si kucheza kwa maelekezo, kila mmoja amepata nafasi ya kuonyesha kiwango chake na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja umeonekana," alisema Mayay

Alisema licha ya kila mmoja kuwa na kiwango bora, lakini kwa upande wake amevutiwa zaidi na kiwango alichoanza nacho Prince Dube nyota wa kigeni wa Azam raia wa Zimbabwe.

"Amekuwa na mchango mkubwa katika kutoa pasi za mwisho 'assist' ukiangalia hata magoli aliyofunga, ni mshambuliaji ambaye binafsi naona ameanza vizuri zaidi ya wengine," alisema.

Kocha Abdallah Kibadeni alisema katika mechi kubwa, Tactical discipline kwa mchezaji ndiyo kila kitu.

"Hivi sasa tunaona wengi wanacheza kwa uwezo binafsi, kila mmoja ameonyesha kiwango bora ni kama mchezo wa wazi, hii imewapa nafasi kila mmoja kuonekana, naona wote wameanza vizuri," alisema.

Advertisement