Sangoma wa Man United kiboko, Cavani naye kaumia

Muktasari:

  • Kabla ya hapo PSG inajulikana kwa utatu mtakatifu wa Mbappe, Neymar na Cavani ambao wamekuwa wakianza mara kwa mara na kutupia mabao mengi katika nyavu za adui mechi za ligi na zile za kimataifa.

PARIS, UFARANSA .KAMA Manchester United inatumia mganga kuelekea mechi yake ya kesho ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya PSG basi inabidi imlipe dau la kutosha. Anaendelea kufanya mambo. Na sasa PSG itamkosa staa mwingine katika pambano la kesho Jumanne, Edinson Cavani.

Kuelekea mechi ya kesho, tayari PSG inamkosa staa wake wa kimatafa wa Brazil, Neymar baada ya mwezi uliopita kuumia vibaya kifundo chake cha mguu, lakini sasa PSG italazimika kumkosa Cavani ambaye ameumia juzi.

Katika pambano la juzi Jumamosi dhidi ya Bordeaux, Cavani aliumia na kuondoka uwanjani akiwa ameshikilia paja lake dakika chache baada ya kuifungia PSG bao katika dakika ya 42 ya pambano hilo ikiwa ni siku tatu kabla ya kucheza na United kesho.

Kama vile haitoshi katika pambano hilo, beki wa kulia wa PSG, Thomas Meunier naye alitolewa nje baada ya kuumia kichwani ikiwa ni muda mchache baada ya kupika bao la kwanza la Cavani katika dakika ya 17 ya pambano hilo.

Na sasa Kocha wa PSG, Thomas Tuchel atalazimika kumpanga mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Kylian Mbappe kama mshambuliaji wa kati huku kushoto akicheza Julian Draxler na kulia Angel Di Maria.

Kabla ya hapo PSG inajulikana kwa utatu mtakatifu wa Mbappe, Neymar na Cavani ambao wamekuwa wakianza mara kwa mara na kutupia mabao mengi katika nyavu za adui mechi za ligi na zile za kimataifa.

Nafuu pekee katika pambano hilo ni kurudi uwanjani kwa kiungo wa kimataifa wa Italia, Marco Verratti ambaye hapo awali alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu. Verratti alicheza kwa saa zima kabla ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo mpya, Leandro Paredes.

Na sasa Verratti anatazamiwa kuanza katika pambano la kesho dhidi ya United ambayo imerudi upya katika fomu yake chini ya kocha wa muda, Ole Gunnar Solskjaer ambaye ameiwezesha kushinda mechi 10 kati ya 11.

Wakati PSG wikiendi iliyopita ikibamizwa kipigo chake cha kwanza katika ligi dhidi ya Lyon huku Solskjaer akiwa uwanjani, United ipo katika mwendo mdundo na juzi iliichapa Fulham mabao 3-0 na hivyo kutinga Top Four huku ikisubiri matokeo ya mechi kati ya Manchester City na Chelsea iliyochezwa jana Jumapili usiku.

Kwa mujibu wa staa wa zamani wa Manchester United, Gary Neville ambaye kwa sasa ni mchambuzi mahiri wa soka England anaamini mechi ya kesho ni miongoni mwa mechi ambazo zitaanza kuamua hatima ya Solskjaer kama anafaa kupewa kazi hiyo moja kwa moja.

“Amekuwa katika mwendo mdundo, kwa sasa ana asilimia sawa ya kupata nafasi hiyo kwa kudumu, anaweza kuwa na asilimia 50 au 60. Lakini mechi dhidi ya Chelsea ugenini (Kombe la FA), PSG katika Ligi ya Mabingwa, Liverpool na nyingine. Kuna changamoto kubwa inakuja ndani ya wiki tano au sita zijazo,” alisema Neville.

“Nadhani mwishoni mwa Machi au mwanzoni mwa Aprili ni muda sahihi wa kupima kazi ambayo imefanywa na Ole. Ameinua morali ya klabu ndani na nje ya uwanja. Ameibadilisha sana na inashangaza,” alisema Neville.

Pambano la marudiano baina ya Manchester United na PSG linatazamiwa kupigwa Machi 3 katika Uwanja wa Old Trafford jijini Manchester na kuna uwezekano Cavani akarudi katika mechi hiyo lakini hakuna uwezekano wa Neymar kucheza mechi hiyo.