Sandumina FC yachota za mezani

Thursday November 8 2018

By Saddam Sadick

KAMATI ya Mashindano ya Chama cha Soka Wilaya ya Magu imeipa ushindi wa mezani Sandumina FC baada ya wapinzani wao, Rugeye Stars kugomea mchezo dakika za mwisho katika mechi ya Ligi Daraja la nne hatua ya nusu fainali.

Mchezo baina ya timu hizo uliochezwa juzi ulishindwa kumalizika dakika ya 78, ambapo kabla ya maamuzi ya Rugeye Stars kugoma kuendelea na mpambano huo timu hizo zilikuwa sare ya mabao 2-2.

Mechi hiyo ilikuwa ya nusu fainali kusaka timu moja ambayo itaungana na Tinsela FC kucheza hatua ya fainali ili kumpata Bingwa wa Wilaya hiyo kupanda Daraja la tatu ngazi ya Mkoa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka wilayani humo (MDFA), Denis Okelo alisema Rugeye waligomea mchezo baada ya mchezaji wao kumuangusha mpinzani wake na mwamuzi kuamuru ipigwe penlati.

Alisema baada ya mvutano baina ya timu hizo kugombea penalti hiyo, viongozi wa Rugeye walitinga uwanjani na kuwataka wachezaji wake kuvua jezi na kuondoka, hivyo kamati ya mashindano kwa kuzingatia kanuni ikaamua Sandumina kupewa ushindi.

“Kutokana na kitendo walichokifanya Rugeye Stars kamati ya mshindano kwa kuzingatia kanuni za Ligi imeamua kuipa ushindi wa pointi tatu Sandumina na kutinga fainali,”alisema Okelo.

Katibu huyo alifafanua kuwa fainali ya kumpata bingwa inatarajia kupigwa Jumapili ya wiki hii na kuondoka na zawadi ya kombe na kitita cha Sh 300,000 huku mshindi wa pili akiondoka na Sh 200,000.

“Hatua ya fainali itachezwa Jumapili na Bingwa siku hiyo atapewa Sh 100,000 mkononi huku kiasi kitakachobaki Chama cha Soka kitailipia ada ya ushiriki ngazi ya Mkoa,”alisema Kiongozi huyo.

Advertisement