Sanchez afunguka kitu Man United

Muktasari:

  • Solskjaer ameongoza kikosi cha Man United kushinda mechi saba mfululizo tangu alipochukua mikoba ya kuinoa timu hiyo mwezi uliopita na kuifanya timu hiyo sasa kuwa nyuma kwa pointi tatu tu kuifikia Top Four ambayo ndio hasa inayotoa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uja

MANCHESTER, ENGLAND.SUPASTAA wa Manchester United, Alexis Sanchez amefunguka akimzungumzia kocha mpya, Ole Gunnar Solskjaer anavyogawa dozi kwa wapinzani kwa sasa.

Mfumo wa kushambulia unaopendelewa na Kocha Solskjaer umemzindua kila mchezaji kwenye kikosi hicho cha Man United na si Sanchez pekee, ambaye ndio kitu anachokipenda anapokuwa uwanjani, kushambulia tu na si kukaba.

Fowadi huyo wa zamani wa Arsenal, Sanchez alisema: “Wachezaji ni wale wanaotumiwa na Solskjaer ndio waliokuwa wakitumiwa na Jose Mourinho. Lakini kwa sasa tumekuwa bora zaidi kwenye kushambulia na tunakaba pia.

“Ukweli ana historia kubwa sana na klabu hii na anapozungumza unahamasika. Falsafa zake ni kugusa mpira mara nyingi zaidi, kutawala mchezo na kufunga mabao.

“Sawa unaweza kusema nafasi yake wakati anacheza ilikuwa kwenye ushambuliaji, lakini bado amekuwa akitaka tuwe makini pia tunapokuwa kwenye eneo letu la penalti. Ndio maana tunapata matokeo mazuri. Kitu ambacho kocha alisema ni kuboresha kiwango ni kazi ya mchezaji mwenyewe.

“Alisema kila kitu kipo kwenye uamuzi wetu na ni suala letu kuhakikisha tunapanda na kushika nafasi za juu kwenye msimamo.”

Solskjaer ameongoza kikosi cha Man United kushinda mechi saba mfululizo tangu alipochukua mikoba ya kuinoa timu hiyo mwezi uliopita na kuifanya timu hiyo sasa kuwa nyuma kwa pointi tatu tu kuifikia Top Four ambayo ndio hasa inayotoa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Kocha huyo hivi karibuni aliwaambia wachezaji wake anataka wapambane na kumaliza ligi wakiwa kwenye nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.