Samatta uso kwa uso na Lukas Podolski

FOWADI wa kimataifa wa Tanzania na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ‘Samagoal’ anatarajiwa kukutana uso kwa uso leo, Jumatatu na mshambuliaji wa zamani wa Arsenal na Bayern Munich, Lukas Podolski.

Wawili hao watakutana huko Antalya, Uturuki kwenye mchezo wa Ligi Kuu nchini humo ‘Super Ligi’ ambao utazikutanisha timu zao kwa mara ya kwanza msimu huu, Samatta atakuwa na chama lake Fenerbahce huku Mjerumani, Podolski akiwa na Antalyaspor.

Huu utakuwa mchezo wa tano wa Super Ligi kwa Samatta ambaye tangu ajiunge na Fenerbahce amekuwa mshambuliaji chaguo la kwanza huku kwa Podolski mwenye miaka 35 ukiwa mchezo wake wa saba msimu huu, akaunti yake ya mabao inaonyesha kuwa na bao moja.

Wakati akaunti ya nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa la Ujerumani kuonyesha kuwa na bao moja ambalo alilifunga Oktoba 24 dhidi ya Basaksehir, amezidiwa bao moja na Samatta mwenye mabao mawili kwenye akaunti yake huku akiwa amecheza michezo michache.

Podolski ni miongoni mwa washambuliaji hatari ambao walitesa Ulaya, alianza kujipatia umaarufu nchini kwao Ujerumani akiwa na FC Koln, Bayern wakamwona na kumsajili, aliichezea klabu hiyo kwa miaka mitatu.

Alivyopoteza namba ya kucheza kikosi cha kwanza cha miamba hiyo ya soka la Ujeruman (Bayern), Koln iliamua kumrejesha nyumbani kabla ya Arsenal kumsajili, alicheza kwa mafanikio makubwa kwa washika mitutu hao wa London lakini kama inavyofahamika soka huendana na umri.

Alisepa zake London, 2015 kwa kwenda Italia kujiunga na Inter Milan lakini hata hivyo huko nako hakudumu, akaiibukia Galatasaray ambao ni wapinzani wa chama la Samatta.

Hakuwa na maisha marefu na klabu hiyo, akaenda zake kuchota pesa za Wajapani na mwishowe akarejea kwenye soka la ushindani kwa kujiunga na klabu anayoichezea hadi sasa (Antalyaspor).

Chama la Samatta litashuka dimbani kwenye mchezo wa leo wakiwa wametoka kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Trabzonspor, presha kubwa inaweza kuwepo kwa Antalyaspor maana wametoka kupoteza kwa mabao 5-1 dhidi ya Istanbul Basaksehir.

NYOTA FENERBAHCE AULA

Klabu ya Fenerbahce ambayo anaichezea Samatta, imempa shavu, Emre Belozoglu ambaye ametundika daruga la kuwa mkurugenzi mpya wa mchezo, Jumatano ya wiki iliyopita.

Taarifa rasmi iliyotolewa na klabu hiyo inaeleza kuwa Belozoglu atakalia kiti hicho kwa makataba wa mwaka mmoja.

“Ni furaha iliyoje kwangu baada ya kumaliza kuichezea kwa mafanikio klabu ninayoipenda halafu napata nafasi ya kuendelea kuwa hapa. Natoa ahadi ya mafanikio, ninachoomba tushikamane,” alisema.