Samatta ukimgusa bao wanamkoma Europa Ligi

Muktasari:

Tangu kuanza kwa msimu huu mshambuliaji huyo amekuwa katika kiwango bora akifunga mabao matano katika mechi za kufuzu kucheza hatua ya makundi Europa Ligi

Dar es Salaam. Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ameendelea kuwa moto wa kuotea mbali katika mashindano ya Europa Ligi baada ya kuifungia KRC Genk bao mmoja katika ushindi wa wa mabao 2-0 dhidi ya Malmo FF ya Sweden kwenye Uwanja wa nyumabani wa Luminus.

Samatta aliyekuwa chini ya ulinzi mkali wa mabeki wa Malmö FF, Lasse Nielsen na Rasmus Bengtsson aliwazidi ujanja na kufunga bao hilo dakika ya 71 huku wakidhani alikuwa ameotea.

Bao hilo lililofungwa na Samatta lilikuwa la pili kwa KRC Genk, bao lao la kwanza kwenye mchezo huo, lilifungwa na Mbelgiji Leandro Trossard dakika ya 37.

Samatta amekuwa Mwafrika wa tano kufunga bao jana katika usiku Europa Ligi, wengine ni Mcameroon, Ismaila  Sarr wa Rennes, Mmali Amadou Haidara (Salzburg), Mcape Verde Jovane Cabral (Sporting CP) na Mgabon  Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal.

Wanaotizamiwa kuwa wapinzani wa kuu kwa KRC Genk kwenye kundi hilo, Besiktas ya Ututuki wanaongoza kundi hilo baada ya kushinda mabao 3–1 dhidi ya Sarpsborg 08 ya Norway.