Samatta staili kama ya Ramos, Ozil

Muktasari:

Katika ndoa hiyo wachezaji wa zamani walihudhuria akiwemo, Kocha wake Zinedine Zidane, nyota wa zamani wa timu hiyo David Beckha, Roberto Carlos na wengine lakini Cristiano Ronaldo ambaye alionekana kuwa swahiba wake alishindwa kwenda baada ya kuonekana Uturuki akifurahia maisha na familia yake.

USIKU wa kuamkia Oktoba 10, nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta aliachana na ukapera na kuamua kuingia kwenye maisha mapya ya ndoa. Hata hivyo, ndoa hiyo ilikuwa na siri sana na wengi iliwashtua maana imekuja ghafla sana.

Samatta ameongeza idadi ndogo ya wachezaji kutoka Tanzania ambao, wameamua kuingia kwenye maisha ya ndoa lakini, ameongeza idadi kubwa kwa wachezaji wanaosakata kabumbu Ulaya.

Miongoni mwa wachezaji walifunga ndoa kwa Tanzania ni beki Abdi Banda, kipa Aishi Manula ambao walifunga ndoa hivi karibuni na sasa wanamkaribisha mkali wao Samatta kwenye chama hicho.

Baada ya kufanya hivyo mshambuliaji huyo wa Genk ameongeza pia idadi ya wachezaji wanaocheza soka Ulaya ambao, wamefunga ndoa mwaka huu na kuanza kufurahia maisha mapya katika ndoa hizo. Makala hii imekuandalia wachezaji wakubwa kutoka Ulaya ambao wamefunga ndoa mwaka huu

Sergio Ramos

Zaidi ya wadau 400 walihudhuria katika Jiji la Seville ambako ndiyo nyumbani kwa beki huyo na kushuhudia alivyokuwa anachukua jiko kwa mara ya kwanza na mke wake Pilar Rubio aliyezaa naye watoto watatu, ambaye ni mtangazaji kituo cha Televisheni cha La Sixta kilichopo Hispania.

Katika ndoa hiyo wachezaji wa zamani walihudhuria akiwemo, Kocha wake Zinedine Zidane, nyota wa zamani wa timu hiyo David Beckha, Roberto Carlos na wengine lakini Cristiano Ronaldo ambaye alionekana kuwa swahiba wake alishindwa kwenda baada ya kuonekana Uturuki akifurahia maisha na familia yake.

Sio Ronaldo tu, golikipa wa zamani wa timu hiyo ambaye ni rafiki yake kipenzi Iker Casillas naye alishindwa kuhudhuria kutokana na matibabu aliyokuwa akipokea Hospitalini kutokana na matatizo ya moyo yaliyoanza akiwa na Fc Porto.

Mesut Ozil

Pengine hii ilikuwa harusi ya funga mwaka nchini Uturuki kutokana na ukubwa wa harusi yenyewe na aina ya watu waliohudhuria katika harusi hiyo.

Ozil amefunga ndoa na Amine Gulse katika jiji la Instanbul na kuhudhuliwa na rais wa nchi hiyo Recep Erdogan.

Ozil 30, amemuoa mwanamke huyo ambaye aliwahi kutwaa taji la Miss Uturuki mwaka 2014, na hata hivyo wawili hao bado hawajabarikiwa mtoto na bila shaka mambo yatakuwa mazuri muda wowote kuanzia hivi sasa tangu alipoo Juni 8, mwaka huu.

Miongoni mwa wachezaji waliohudhuria ndoa hiyo ni pamoja na rafiki yake wa karibu ambaye ni mchezaji mwenzake Sead Kolasinac pamoja na baadhi ya wachezaji akiwemo Aaron Ramsey na Granit Xhaka.

Harry kane

Nyota huyo wa Totenham Spurs ni mfano wa kuigwa na wengi ameoa mwanamke ambaye alikuwa rafiki yake tangu kipindi cha utoto wao.

Baada ya kukuwa waliamua kuanza mahusiano na kupata mtoto mmoja anayeitwa Ivyjane Kane mtoto huyo akiwa na mwaka mmoja pekee Harry Kane aliongeza mwingine Vivienne Jane Kane

Mkali huyo wa mabao mwenye miaka 26, amefunga ndoa katika ukumbi wa sherehe wa Lavish uliopo England na kuhudhuriwa na mchezaji wa zamani wa taifa hilo Jamie Redknapp na baadhi ya nyota wa Totenham akiwemo Dele Ali na Eric Dier.

Harry Kane na Kate Goodland baada ya muda mrefu kutengena walirudiana tena mwaka 2017 na hapo ndipo safari ya mahusiano yenye umakini yalianza rasmi baada ya kupata watoto wawili ndani ya miaka miwili walifunga ndoa Juni 21 mwaka huu.

Mbwana Samatta

Samatta amemuowa mpenzi wake Naima Omary, ambaye tayari ana watoto wawili aliozaa na nahodha huyo wa Taifa Stars miaka kadhaa iliyopita.

Washikaji zake, Himid Mao na Thomas Ulimwengu walikuwa miongoni mwa wachezaji waliohudhuria ndoa hiyo.

Henrick Mkhitaryan

Kiungo huyo anayekipiga As Roma kwa mkopo akitokea Arsenal amefunga ndoa na mpenzi wake Betty Vardanyan mtoto wa mfanyabiashara mkubwa kutoka nchini Armenia Mikael Vardanyan ambaye aliachiwa urith na baba yake Hrant Vardanyan aliyefariki Dunia 2014 nchini Armenia.

Wawili hao wenye miaka 30, walifunga ndoa hiyo ya kifahari na kufuirahia maisha kwenye boti muda mchache baada ya kufungishwa ndoa hiyo.

Mkhitaryan alianza kuwa na uhusiano na mwanake huyo mwaka 2018 na hapo alianza harakati za kufunga ndoa na hatimaye alifanikisha mwaka huu.

Hao ni miongoni mwa wachezaji wakubwa walioagana na ukapela na kuamua kuingia kwenye maisha ya ndoa kwa mara ya kwanza na wengine wameingia kwenye maisha hayo wakiwa tayari na watoto kuanzia wawili akiwemo Sergio Ramos na Mbwana Samatta.

Wapo wachezaji wengine ambao wamefunga ndoa miaka ya hivi karibuni na miongoni mwao ni kiungo wa Juventus Aaron Ramsey, kiungo wa Arsenal Granit Xhaka, Adres Iniesta , Xavi Hernandez, Hamza MendyI Schalker04 na Hirving Lozano wa PSV.