Samatta rekodi zake tamu zamtikisa mghana

Muktasari:

  • Leo tunaendelea na mfululizo huo tukiangalia namna Samatta tangu alipotua Genk na rekodi alizoziandikisha sambamba na rafiki yake mwenye asili ya Ghana anavyomzungumzia.

KATIKA mfululizo wa makala kuhusu Mbwana Samatta, nyota wa Kimataifa wa Tanzania anayekipiga klabu ya Genk, jana tuliona namna dau lake linavyoweza kuinunua Simba yote na chenji ikabaki.

Ndio, thamani iliyowekwa kwa Samatta kwa sasa ni ya Sh 23.7 bilioni, ambazo ni zaidi ya fedha ambazo Mohammed Dewji amezitoa ili kuwa mwekezaji wa Simba.

Chenji inayobaki unasajilia timu mbili za Simba kwani inaelezwa thamani ya kikosi cha sasa ni Sh 1.3, ikiwa na maana kwa vikosi viwili ni Sh 2.6 tu ambazo ni pungufu mbele ya salio linalobaki la Sh 3.7 bilioni iliyosalia baada ya kutoa Sh 20 bilioni za MO Dewji za kumilikiwa klabu.

Leo tunaendelea na mfululizo huo tukiangalia namna Samatta tangu alipotua Genk na rekodi alizoziandikisha sambamba na rafiki yake mwenye asili ya Ghana anavyomzungumzia.

Endelea naye...!

REKODI KIBAO

Kati ya rekodi tamu zilizowekwa na Samatta kwa sasa ni kuwa kwenye orodha ya washambuliaji wenye mabao mengi Ulaya inayoongozwa na staa wa Barcelona, Lionel Messi.

Messi anaongoza kwa kufunga jumla ya mabao 34 kwenye mashindano yote Ulaya, akifuatiwa na Samatta na Kylian Mbappé wa PSG ambao kila mmoja akiwa mabao 29.

Samatta amefunga mabao 20 katika Ligi Kuu ya Ubelgiji akiwa ndiye kinara na kuiweka timu yake kileleni, lakini pia ana mengine 9 aliyofungwa kwenye Ligi ya UEFA Europe League.

Pia Samatta anashika nafasi ya tano kwenye orodha ya wafungaji wa muda wote wa Genk akiwa na mabao 63 (kabla ya mechi yao ya jana), nyuma ya Elyaniv Barda aliyetundika daruga akiwa na mabao 67 aliye nafasi ya nne, anayeongoza Jelle Vossen mwenye mabao 105 anayeichezea Club Brugge.

USAJILI WAKE GENK

Baada ya kushinda tuzo, Januari 2016 ya Mwanasoka Bora kwa Wachezaji wa ndani ya Afrika enzi hizo akiwa TP Mazembe ya DR Congo, zilianza fununu za Samatta kutakiwa na klabu kubwa Ulaya.

Kweli kama utani, alijiunga na KRC Genk akitokea Mazembe kwa kitita cha Euro laki tano ambazo ni zaidi ya bilioni 1.3 kwa fedha za Kitanzania.

Mara baada ya kutua Genk, Samatta alitoa gundu kwa kuifungia klabu yake hiyo mpya bao lake la kwanza Februari 28, 2016 kwenye mchezo dhidi ya Club Brugge ambao waliibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Upande wa mabao matatu kwa mara ya kwanza yaani hat trick aliifunga Agosti 23 mwaka jana kwenye mchezo dhidi ya Brøndby IF wa Europa Ligi ambao waliishinda mabao 5-2.

HUYU NDIYE SAMATTA

Mbwana Ally Samatta, alizaliwa Desemba 23 1992, alianza kucheza soka la mtaani, Mbagala Market kisha African Lyon na Simba ambako alijipatia umaarufu nchini na baadae TP Mazembe ya DR Congo kabla ya KRC Genk ya Ubelgiji.

Kabla ya kuonwa na TP Mazembe mwaka 2011, Samatta alikuwa nje ya uwanja wa muda wa miezi kama sita akishinikiza kutimiziwa ahadi ya kununuliwa gari kama sehemu ya usajili.

Simba ilimuahidi fedha na gari kama sehemu ya usajili, alipoona wanamzingua alisalia nyumbani, lakini viongozi waliamua kutii msimamo wake na kumpa gari na kuanza kucheza.

Moto aliouwasha uliwafanya Wakongo ambao waling’olewa katika Ligi ya Mabingwa msimu huo kwa kosa la kucheza mchezaji asiyestahili walitoa Dola 150,000 kumbeba jumla.

NYOTA YA UONGOZI

Unaweza kudhani kuwa ni utani, lakini ndivyo hivyo tena, unaambiwa nahodha huyo wa Stars, Samatta ni kama Rais wa Genk kutokana na makubwa aliyoifanyia klabu hiyo.

Tukirejea nyuma ni kwamba katika masuala ya uongozi, Samatta alianza kujiwekea tangu akiwa Simba ambapo alimkuta Mussa Hassan Mgosi aliyekuwa mfalme katika klabu hiyo lakini kwa kipindi kifupi aliuangusha utawala huo na kuweka wake.

Licha ya kuwa Mgosi ndiye mchezaji ambaye wakati Samatta akiwa African Lyon na hata Mbagala Market alikuwa akitamani kufikia mafanikio ya mkali huyo ambaye kwa sasa ni kocha wa kikosi B cha Simba.

Alipotua TP Mazembe, Samatta alikutana na utawala Trésor Mputu ambaye alikuwa kipenzi cha bosi wa timu hiyo, Moïse Katumbi kama kawaida yake alianza mdogo mdogo na mwishowe akageuka kuwa mfalmwe kwenye klabu hiyo.

MSIKIE SWAHIBA WAKE

Gazeti hili lilipata nafasi ya kuongea na kinda la Kighana ambaye ametokea kuwa swahiba mkubwa wa Samatta ndani ya Genk. Kinda huyo, Joseph Paintsil ametudokezea kwa kusema Samatta ni mfano mzuri kwao wanaochipukia na wamekuwa wakimuona kama rais kwenye klabu yao.

Paintsil ni miongoni mwa makinda ambao kocha, Philippe Clement amekuwa akitoa nafasi ya kutosha kwao kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

“Hapa tunamwita Rais, ni kweli ni Rais wetu amekuwa akiifanya kazi kuwa nyepesi kwenye michezo migumu ambayo tumekuwa na uhitaji wa matokeo,” anasema Mghana huyo.

SAMATTA NDIYE ALIYEMPOKEA

“Samatta ni kaka kwangu, yeye ni Mwafrika mwenzangu na ni mchangamfu kwa hiyo ilikuwa rahisi kuwa naye karibu.

“Nimemkuta akiwa mchezaji wa kutegemewa kwenye kikosi cha kwanza, nilikuwa nikitumia muda wangu mwingi kuwa naye karibu ili nijifunze baadhi ya vitu ambavyo nilikuwa nikiamini vitanisaidia. “Kabla ya kuja huku nilimjua Samatta kupitia Youtube, nilikuwa napenda sana kuangalia nani mchezaji hatari zaidi na nilibaini hilo kwa namna alivyokuwa akifunga mabao,” anasema

ACHOCHEA NDOTO

Paintsil anasema ndoto yake ni kuwa mchezaji muhimu kuanzia kwenye kikosi chake cha Genk hadi timu ya taifa lake la Ghana kama ilivyo kwa Samatta ambaye amekuwa akifanya vizuri pande zote mbili. “Ghana kuna wachezaji wengi wenye uwezo na uzoefu wa kutosha ila nachoamini ni kwamba utafika muda wa kutegemewa na kuwa mchezaji muhimu kwenye taifa langu.”

MAJONZI YAANZA KUTAWALA

Winga huyo wa kushoto, anasema endapo Samatta akiondoka Genk majira ya kiangazi, watasikitishwa na uamuzi wake huo lakini watauheshimu na kumtakia kila la kheri.

“Kiukweli tumemzoea sana Samatta, itatuchukua muda kuzoea maisha bila yeye, kila mchezaji kwa sasa ameanza kuwa simanzi baada ya kusikia kuna timu zinataka kumchukua. Tumemzoea.”

Je unajua kama Samatta anaye shabiki wa kudumu ambaye amekuwa akimfuailia tangu akiwa nyumbani na sasa wanaishi wote nchini Ubelgiji na huwa hakosi kumshuhudia uwanjani?

Shabiki huyo ni nani na ilikuwaje hata akaangukia kwa Samatta na sio wachezaji wengine? Endelea naye kesho Jumatano.