Samatta na Msuva wamefanya haya

Muktasari:

  • Simon Msuva amesema Tanzania inanafasi kubwa ya kufuzu kushiriki Afcon mwakani kwa vile Stars wamechoka kuwa wasindikizaji na ameomba sapoti kutoka kwa watanzania wote kuendelea kuiombea timu yao na kuipa ushirikiano katika hali zote  tukiwa tumeshinda na tukiwa tumefungwa pia.

WAHENGA wanasema heri nusu shari kuliko shari kamili, ushindi wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Taifa ya Cape Verde siku ya Jumanne si haba kwani umeiweka katika nafasi ya pili.

Uwepo nafasi ya pili katika kundi L’ linaloongozwa na Uganda unaiweka Taifa Stars katika nafasi nzuri ya kusaka tiketi ya kwenda Afcon hapo mwakani

Mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa ilishuhudia, Mbwana Samatta akikosa penati lakini alibaki kuwa shujaa wa mchezo huo, kwani alitengeneza nafasi ya goli la kwanza lililofungwa na Simon Msuva kisha akafunga bao la pili.

Samatta ambaye ni nahodha aliondoka mara baada ya mchezo huo kwenda Ubelgiji kuitumikia Klabu ya K.R.C. Genk na Msuva atarudi Morocco kuitumikia klabu yake ya Difaâ El Jadidi na huku wengine watarudi katika klabu zao hapa nyumbani.

Wachezaji wote wa timu ya taifa walioshiriki mechi ya jumanne wanakabiliwa na hali ya uchovu wa mwili, hii ni kutokana na kutumia nguvu nyingi kuhakikisha wanapata ushindi. Lakini kwa Msuva na Samatta watakabiliwa na uchovu mwingine wa safari kutokana na kusafiri umbali mrefu kwa ndege kurudi katika klabu zao.

Wachezaji hawa watahitaji kufanya kila wanaloweza kuepukana na uchovu huo wa mwili, watahitaji kufanya mbinu za kitabibu ili kurudi upya na nguvu.

Lengo la kufanya hivyo ni kuweza kucheza kwa kiwango chenye ushindani bila kuchoka, leo tutaona mambo yanayofanyika ili kuweza kuondokana na hali ya uchovu wa viungo vya mwili ikiwamo misuli.

UCHOVU WA VIUNGO VYA MWILI NI NINI?

Kitabibu Uchovu hujulikana kama ‘Muscle fatigue au Physical fatigue’ ni hali inayojitokeza mwilini pale misuli ya mwili inapofanyishwa kazi kupita kiwango chake.

Ukiwauliza wachezaji wetu wa timu ya taifa mara baada ya mechi ile, kesho yake asubuhi walipooamka watakuambia kuna hali ya maumivu ya viungo iliwapata hii ni kutokana na misuli yao kufanya kazi sana.

Tatizo la kuambatana na maumivu huwa ni kawaida kwani ndiyo kama ishara ya mwili kujihami kuwa misuli imefanya kazi kupita kiwango chake.

Uwepo wa uchovu mwilini unasababisha misuli ya mwili kukosa nguvu kama ilivyo kawaida yake kwani maumivu hayo huwa ni kama pingamizi la utendaji kazi wa misuli.

Ndiyo maana mchezaji mwenye uchovu usioisha hucheza chini ya kiwango na katika timu zilizopiga hatua kama wanazocheza kina Samata ni lazima hatua madhubuti zichukuliwe kulikabili tatizo hili.

Uchovu unapoambatana na maumivu ya mwili unaweza kuwa na matokeo ya maumivu yanayoweza kuwa ya kawaida, ya kati mpaka ya juu.

Uchovu unatokana na uwapo wa vitu vinavyoingilia hatua za misuli za kukunjuka na kujikunja pale viungo hivi vinapofanya mijongeo mbalimbali ikiwamo kukimbia kwa kasi.

Tatizo la uchovu linaweza kusababishwa na mishipa ya fahamu kutosisimua vizuri misuli na pamoja na mrundikano wa mabaki baada ya seli za mwili kutumia sukari ya mwili kupita kiwango chake.

Je unaukabili vipi uchovu?

Uchovu unaotokana na mwili kufanya kazi sana ni tatizo la muda, ambalo linaweza kuisha na mchezaji kurudi na nguvu mpya.

Wachezaji wanaweza kupata uchovu zaidi kwa kucheza mechi ngumu, kutokunywa maji mengi kabla na baada ya mechi, kucheza katika joto kali, kutopasha na kunyoosha viungo, lishe duni, kutopumzika, kusafiri umbali mrefu na kufanya mazoezi magumu kabla ya mechi.

Mara tu baada ya kumaliza mechi kama ile inatakiwa wachezaji wanywe maji mengi kwani imechezwa kipindi hiki cha joto kali hivyo wachezaji wanapoteza maji mengi kirahisi.

Tuliona makala ya wiki iliyopita namna upungufu wa maji na chumvi unavyoathiri misuli ya wachezaji kwa kuchangia kupata uchovu wa misuli.

Wachezaji hutakiwa kunywa maji mengi na matunda, juice za matunda au vinywaji maalum vijulikanavyo kama ‘Sports Drinks’ muda mfupi baada ya kumaliza kucheza.

Inashauriwa angalau kunywa lita moja na nusu ya maji baada ya mechi ili kurudishia kiwango cha maji kilichopotea wakati wa kucheza huwa na tija endapo maji hayo yatakuwa yakawaida au vuguvugu.

Huitajika kufanya mazoezi mepesi yakunyoosha misuli ya mwili unasaidia kukabiliana na uchovu angalau kwa dakika 5-10, mazoezi haya yafanyike mchezaji akiwa katika ulalo sahihi ili asijeruhi misuli.

Usingaji wa mwili (massage) ni mbinu mojawapo ya kuondokana na uchovu wa mwili kwani inawezesha mishipa ya damu kutanuka, hivyo damu kwenda kwa wingi katika misuli hivyo kuondoa uchovu kirahisi.

Mchezaji anaweza kuoga maji ya vuguvugu au katika mabafu yakisasa yenye kutoa mvuke wa joto au barafu.

Mchezaji atahitajika kupumzisha mwili katika maeneo yenye hewa safi ya wazi au ufukwe, kupumzika katika nyumba ambazo hazipo katika msongamo ikiwamo ufukweni au maeneo ya wazi.

Kumbuka kuwa Mazingira ya hewa chafu yanachangia kuongeza uchovu wa mwili kwani misuli inahitaji kutumia hewa safi yenye Oksijeni ili kuondoa uchovu.

Hutakiwa kula mlo kamili ikiwamo vyakula vyenye protini, mboga za majani, matunda na wanga kwani inasaidia kukurudishia nguvu iliyotumika na pia kurudishia akiba ya nishati katika misuli. Protini ndio mlo unaowezesha misuli kujijenga na kufanya kazi yake kwa ufanisi na pia inatumika katika misuli wakati wa kukunjuka na kujikunja.

Mlo wa jioni au usiku huliwa masaa 2-3 kabla ya kulala kwani kula tu na kulala kunasababisha kuamka na uchovu hii ni kwasababu mwili unatumia muda mwingi kusaga chakula badala ya kujikarabati. Kulala ni moja ya tiba nzuri ya uchovu, mchezaji huitajika kulala masaa 6-8 mfululizo kwa usiku mmoja pasipo usumbufu wowote.

Hutakiwa kuepuka kupata msongo wa mawazo, sonona (depression) na shinikizo la kiakili kwani mambo haya ni hisia hasi ambazo zinaongeza uchovu wa mwili.

Hutakiwa kuepuka matumizi ya unywaji pombe kupita kiasi, matumizi ya tumbaku ikiwamo uvutaji sigara kwani vyote hivi vinachangia kuongeza uchovu wa mwili.

Msuva na Samatta watasafiri umbali mrefu mara baada ya kufika wataendelea kufanya mambo haya au zaidi ili kuondokana na uchovu na kurudi na nguvu mpya.