Samatta kutua Galatasaray ni suala la muda tu

Muktasari:

Kiwango cha juu alichokionyesha Samatta katika msimu uliopita akiwa na Genk kimezivutia klabu nyingi barani Ulaya

Dar es Salaam. Wawakilishi wa mabingwa wa Ligi Kuu Uturuki, Galatasaray wapo jijini Genk katika mazungumzo ya kukamilisha uhamisho wa mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta.

Mtandao wa CNNTURK pamoja na mitandano mingine ya Uturuki vimeripoti taarifa ya msafara wa Galatasaray kuwa kati majadiliano na uongozi wa Genk na lolote linaweza kutokea leo.

Samatta amerejea Genk jana alifanyia vipimo vya afya hata hivyo hatma yake ndani ya klabu hiyo bado ni swali linaloendelea kuumiza vichwa.

Kwa muda gani Samagoal ataendelea kuwa mchezaji wa Genk ni swali zuri linalosubiri jibu magazeti mbalimbali ya Uturuki yameripoti leo taarifa ya Galatasaray kuingia katika mbio za kumsaka nyota huyo wa Tanzania.

Leo viongozi wa Galatasaray wamefika Luminus Arena kwa lengo moja la kufanya majadiliano juu ya uhamisho wa mchezaji huyo.

Galatasaray ni mabingwa wa Ligi Kuu Uturuki wapo chini ya kocha Fatih Terim wapo tayari kutoa euro 10milioni kwa ajili ya kumnasa Samatta.

Msimu uliopita, Samatta alifunga mabao 32 katika mechi 51 alizocheza katika klabu yake ya Genk na kuisaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ubelgiji.

Mbali ya Galatasaray timu nyingine zilizoonyesha nia ya kumtaka Samatta ni pamoja na Leicester, Aston Villa, Burnley na Watford zote za England.