Samatta bado saa tu unaambiwa

Muktasari:

Unaambiwa mashabiki wapatao 1000 wamesafiri kwenda Bruges kuisapoti KRC Genk anayoichezea Samatta ili iweze kufanya kweli kwenye mchezo huo ambao utachezwa majira ya saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

NYOTA wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta kwa sasa anahesabu saa tu kabla ya kuandika rekodi mpya kwake ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Ubelgiji msimu huu.
Samatta anayeongoza kwa mabao katika ligi hiyo ikiwa hatua ya play-off, anatrajiwa kuiongoza timu yake ya KRC Genk kuvaana na Club Brugge ugenini na kama itashinda itabeba taji.
Nahodha huyo wa Taifa Stars, atasafiri na Genk umbali wa Kilometa 191 kutoka mji wao wa Genk hadi Bruges kucheza mechi hiyo na matokeo mazuri kwao itawapa taji la nne.
Samatta aliye mshambuliaji tegemeo wa klabu hiyo anatarajiwa kukutana na upinzani mkali kutoka kwa Brandon Mechele na Benoît Poulain ambao wamekuwa wakicheza mara kwa mara kama mabeki wa kati wa Brugge.
Mchezo huo ni wa nane kwao, huku Genk ikiiwa kileleni na alama zao 50, sita zaidi ya walizonazo wenyeji wao wenye pointi 44.
Sare au ushindi kwa Genk katika mchezo huo, kutakuwa na utofauti wa pointi ambao hakuna timu yoyote inayoweza kuzifikia hata kama watapoteza michezo miwili zitakazosalia.
Kama wakishinda au kutoa sare hii itakuwa awamu ya kwanza kwao kutwaa ubingwa huo tangu msimu wa 2015/16 Ligi yao ilibadilishwa jina na kuwa Ligi Kuu badala ya daraja la kwanza.
Mara zao tatu ambazo wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ubelgiji kipindi hicho, 1998–99, 2001–02, 2010–11 huku wakimaliza nafasi ya pili, mara mbili kwenye msimu ya 1997–98, 2006–07.

KIJIJI CHAMFUATA SAMATTA
Unaambiwa mashabiki wapatao 1000 wamesafiri kwenda Bruges kuisapoti KRC Genk anayoichezea Samatta ili iweze kufanya kweli kwenye mchezo huo ambao utachezwa majira ya saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Samatta aliyefunga mabao 23 ataingoza Genk akitoka kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka Ubelgiji mwenye asili ya  Afrika 2019 ‘Ebony Shoe’.