Samatta aziingiza vitani Everton, West Ham

Muktasari:

Nahodha Samatta ataiongoza Taifa Stars katika mechi mbili dhidi ya Cape Verde ameanza vema msimu huu wa ligi barani Ulaya hadi kuzivutia timu kadhaa zinazomfuatilia.

Dodoma. Nyota ya mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania na KRC Genk, Mbwana Samatta imezidi kung’ara baada ya kuiziingiza vitani miamba Ligi Kuu England, Everton na West Ham.

Samatta msimu huu amekuwa katika kiwango bora cha kuzifumania nyavu jambo lililozivutia klabu kadhaa kubwa barani Ulaya zikiwamo Everton na West Ham ambazo zimeanza jitihada za kumsajili.

Everton inatajwa kumlenga Samatta kwa lengo la kwenda kuziba nafasi ya mshambuliaji wake Oumar Niasse anayetajwa kuondoka katika timu hiyo katika dirisha la usajili wa Januari nchini England.

Kocha wa Everton, Marco Silva inaelezwa amevutiwa na kasi ya ufungaji mabao wa Samatta hivyo amemuweka katika rada za wachezaji anaowahitaji dirisha dogo mwakani.

Mbali na Everton na West Ham timu nyingine za Ligi Kuu England zilizotajwa kumfuatilia Samatta ni pamoja na Brighton na Burnley.

Samatta ameuanza msimu huu kwa kasi ya aina yake amefanikiwa kufunga mabao 14 katika michezo 16 aliyocheza hadi sasa katika Ligi Kuu ya Ubelgiji na Europa Ligi.