Samatta awekwa mtu kati Ubelgiji

Muktasari:

  • Vita hiyo imepamba moto kufuatia Samatta naye kujibu mapigo Jumamosi kwa kupachika bao kwenye sare ya bao 1-1 ambayo KRC Genk imetoka na Kortrijk kwenye uwanja wa nyumbani wa Luminus.

UNAWEZA kusema ni kama nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anachangiwa kwenye mbio za kuwania kiatu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu Ubelgiji kutokana na wapinzani wake wakuu, Landry Dimata na Ivan Santini kucheza timu moja.

Mbelgiji Dimata ambaye ni mzaliwa wa DR Congo na Mcroatia, Santini ni washambuliaji ambao wanafanya vizuri na kutegemewa kwenye kikosi cha Anderlecht ambacho kinamataji 34 ya Ligi Kuu ya Ubelgiji.

Wiki kadhaa nyuma Samatta alikuwa kinara wa mabao kwenye Jupiler Pro, akiwa na mabao 10 huku nyuma yake wakija kwa kasi wapinzani wake hao, Dimata na Santini.

Kabla ya kutulia vizuri akiwa na mchoro wake mgongoni wa ng’ombe wa dhahabu kutokana na kuwa kwake kinara wa mabao, Dimata ambaye ni mzaliwa kwenye taifa hilo, amemfikia kwenye idadi ya mabao aliyokuwa nayo (10).

Ndani ya michezo minne mfululizo iliyopita dhidi ya Club Brugge, Royal Excel Mouscron, Cercle Brugge, Sporting Charleroi na Anderlecht ambayo Samatta hakufunga, Santini aliyekuwa nyuma akampiku nahodha huyo wa Stars bao moja kwa kuwa na mabao 11.

Vita hiyo imepamba moto kufuatia Samatta naye kujibu mapigo Jumamosi kwa kupachika bao kwenye sare ya bao 1-1 ambayo KRC Genk imetoka na Kortrijk kwenye uwanja wa nyumbani wa Luminus.

Bao hilo limemfanya Samatta kufikisha mabao 11 msimu huu kwenye Jupiler Pro sawa na Mcroatioa, Ivan Santini wa Anderlecht ambaye jana, Jumapili alikuwa mzigoni na mwenzie Dimata kuiongoza timu yao kucheza dhidi ya Charleroi S.C.