Samatta atoboa kilichoawaangusha kwa Liverpool

Muktasari:

Samatta anakibarua kizito mbele yake cha kuhakikisha  KRC Genk wanafanya vizuri kwenye michezo mingine mitatu ya marudiano  iliyosalia katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya taifa 'Taifa Stars' na klabu ya KRC Genk, Mbwana Samatta amesema uzoefu ndiyo uliochangia kupokea kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Liverpool katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Samatta alisema uzoefu wa Liverpool katika Ligi hiyo ya Mabingwa Ulaya ilikuwa moja ya sababu zilizowafanya kupoteza mchezo huyo licha ya kucheza kama timu.

"Tulijiandaa kucheza vizuri, lakini mambo hayakuwa mazuri upande wetu. Kuna muda unatakiwa kujifunza kutokana na kile ambacho kimetokea, nina imani tutasimama upya na kwenda kupigania matokeo ya ushindi Anfield," alisema nahodha huyo.

Samatta mwenye bao moja katika mashindano hayo, alipachika bao lililokataliwa dhidi ya Liverpool baada ya kubainika kuwa alizidi kabla ya kupigiwa krosi, aliyoimalizia kwa kichwa mbele ya James Milner.

Kabla ya mchezo wa jana, kocha wa KRC Genk, Felice Mazzù alisema kuwa Liverpool ni timu bora kwa sasa duniani.

Huku upande wa kocha wa Liverpool, Klopp akisema, "Ni timu nzuri ambayo imekuwa ikicheza kwa kushirikiana huku wakitumia mawinga kushambilia."

Kwa matokeo ya ujumla kwenye Kundi E, wanaoongoza ni Napoli wenye pointi saba, wanaofuata ni Liverpool wakiwa na pointi sita huku wakifuata, Salsburg wenye pointi nne, Genk wanaburuza mkia wakiwa na pointi moja.